Mjadala umezuka nchiniRwanda ambapo baadhi ya wananchi wanataka kurejeshwa kwa hukumu ya kifo nchini kufuatia kesi dhidi ya mwanamme mmoja, mtumishi wa nyumbani, anayetuhumiwa kumuua mtoto wa kike kwa kumkata kichwa.Rwanda haina hukumu ya kifo na baadhi ya wananchi wameelezea haja ya serikali kufanya marekebisho ya sheria ili kuirejesha hukumu hiyo.Kesi dhidi ya mwanamume huyo awali iliendeshwa hadharani katika uwanja wa mpira mjini Kigali na polisi walikuwa na wakati mgumu kumlinda dhidi ya watu waliokuwa na hasira waliotaka auwawe. Mamia ya watu walijitokeza kwenye uwanja wa michezo wa Nyamirambo kushuhudia kesi iliyofanywa hadharani kwa mara ya kwanza. Mamia ya watu walijitokeza kusikiliza kesi inayomkabiliwa Sylivester Hola, ambaye alimuua msichana mwenye umri wa miaka 12, aliyekuwa binti wa mwajiri wake, ambaye amemfanyia kazi zaidi ya miaka 10. Maafisa wa polisi walikuwa na muda mgumu kujaribu kuwazuia watu waliotaka kumwadhibu mtu huyo wenyewe. Raia mmoja wa Rwanda, ambaye hakutaka jina lake kutajwa aliiambia BBC kuwa hukumu ya kifo ni sharti irejeshwe: "mtu anayeua kwa kisu anapaswa kuuawa kwa risasi au apigwe risasi na auwawe ili uwe mfano kwa watu wengine kama yeye," mtu huyo alisema.