Polisi nchini Nigeria wanasema kuwa shule ya mabweni ya wasichana imeshambuliwa katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo huku wasichana wakitekwa nyara. Wazazi wanasema kuwa zaidi ya wasichana miambili wametekwa nyara na washambuliaji hao.Washambuliaji wanaaminika kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram. Utekaji nyara huo ulifanyika usiku wa manane katika shule ya Chibok ksuini mwa mji wa Borno , karibu na mpaka na Cameroon.

Inaarifiwa wasichana 300 walikuwa wanajiandaa kwa mitihani yao. Mmoja wa wasichana alifanikiwa kutoroka na aliambia BBC kuwa walikuwa wanalala wakati walipovamiwa na wanaume waliokuwa wamejihami.

Waliowashambulia wanaaminika kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram.
Wanaume hao waliingiza magunia ya chakula katika malori yaona kuwaamuru wasichana kuyapanda malori hayo.

Wasichana 15 walifanikiwa kutoroka baada ya lori walimokuwa kukumbwa na hitilafu.

Wakazi wa kijiji cha Chibok wanasema kuwa walisikia milipuko kadhaa huku nyumba 170 zikiteketezwa.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa wanajeshi wawili waliuawa huku mali ikiharibiwa wakati wa shamblizi hilo mjini Chibok.
Mnamo siku ya Jumatatu, zaidi ya watu 70, waliuawa katika milipuko miwili ya mabomu katika kituo cha mabasi mjini Abuja.
Kundi la Boko Haram pia limelaumiwa kwa kufanya shambulizi hilo.