Virusi sugu vya HIV
Kuna uwezekano kuwa janga la ukimwi huenda likadhibitiwa ifikapo mwaka 2030, kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi.


Ripoti hiyo imesema kuwa idadi ya visa vya maambukizi mapya na vifo kutokana na HIV, vimeendelea kushuka.Hata hivyo, shirika hilo linataka juhudi zaidi za kimataifa kufanywa kwani za sasa hazitoshi
Na shirika la misaada la Medecins Sans Frontieres limeonya kuwa watu wanaoishi na virusi hivyo hawapati dawa za kutosha.
Kwa mujibu wa shirika hilo watu milioni 35 wanaishi na virusi vya HIV.
Ripoti hiyo ilionyesha visa vipya vya maambukizi milioni 2.1 vilitokea mwaka 2013. Idadi hii iko chini kwa asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka 2001.
Vifo kutokana na HIV pia vimepungua kwa asilimia 5 katika miaka mitatu iliyopita. Kwa sasa watu milioni 1.5 hufariki kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.
Afrika Kusini na Ethiopia zimepiga hatua katika kupunguza vifo vya wagonjwa wa HIV.