“Ni muhimu  kudumisha amani nchini, tusizipe nafasi tofauti zetu za kidini kwani tusipokuwa waangalifu tunaweza kusababisha mvurugano katika jamii yetu” Alhaj Mussa Salum 

Dar na Mikoani. Karibu katika kila mkusanyiko wa swala ya Idd el Fitri, neno “Katiba” lilitajwa wakati viongozi wa dini ya Kiislamu walipokuwa wakitoa mawaidha yao ya sikukuu hiyo kusherehekea kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Mfungo wa Ramadhani.
Katika mahubiri hayo, viongozi hao wa kidini walitaka mchakato wa Katiba uzingatie masilahi ya umma.
Mahubiri hayo yamekuja zikiwa zimebaki siku saba kabla ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kuendelea mjini Dodoma, lakini kukiwa na sintofahamu kutokana na wajumbe wanaounda Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao kwa madai ya kutozingatiwa kwa maoni yaliyotolewa na wananchi.
Ukawa wanadai mjadala wa Katiba ni lazima ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na hali kadhalika kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha.
Jijini Dar es Salaam, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kuweza kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya Katiba.
Katika salamu zake za Idd, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Suleiman Lolila alisema tayari fedha nyingi za umma zimeshatumika kuandaa mchakato wa Katiba Mpya, hivyo siyo busara kususia mchakato wake katika hatua zake za mwisho.
“Baraza linawasihi waliosusia warejee bungeni kwa sababu gharama kubwa zimeshatumika na kama kuna tofauti ziende zikajadiliwe na kumalizwa ndani ya Bunge,” alisema Lolilo.
Aliongeza kuwa Baraza linasikitika kwani maoni ya Waislamu hayakutiliwa maanani katika kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya na kwamba wanaamini yatazingatiwa katika hatua zinazofuata za mchakato huo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akihutubia Baraza la Idd jijini Dar es Salaam, alisema  mchakato wa Katiba Mpya una lengo zuri kwa masilahi ya taifa na katika mtikisiko ambao wamepitia hadi sasa ni vyema ukafikia mwisho na maelewano yapatikane.
“Walioko nje ya Bunge nawaomba warudi ndani kwani huko ndiko tunakoweza kujadiliana, tukatofautiana na kufikia hatua kufika makubaliano na nashukuru hata viongozi wa dini mmeligusia hilo,” alisema Pinda.
Alieleza kwamba kwa sasa kilio cha Watanzania wengi ni kuona Bunge la Katiba likiendelea kwa wale walio nje kurudi ndani kisha kujitazama upya na kupitia kuhusu udhaifu wote wa Katiba ya zamani na kurekebisha kwa ajili ya kupata Katiba nzuri itakayotupeleka mbele kwa miaka mingine mingi ijayo.
Naibu Kadhi, Masheikh
Naye Naibu Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Aboubakar Mdee katika salamu zake, alisema ushirikiano ni jambo muhimu katika maisha ya binadamu na ili nchi ipate mafanikio inahitaji nguvu za pamoja za wananchi wote.
“Bila kuangalia tofauti zetu za kiimani na kimaumbile, hii itasaidia kuijenga nchi katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na pia kuitoa nchi katika matabaka yanayoweza kusababisha migongano isiyokuwa na tija,” alisema.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani nchini na kwamba tofauti za kidini zisipewe nafasi kwani zinaweza kuvuruga jamii.
Salum, aliyekuwa akitoa hotuba ya Idd baada ya swala iliyoongozwa na Sheikh Ally Muhidin Mkoyogole, alisema Uislamu ni dini inayoheshimu haki za binadamu na hakuna Mwislamu ambaye anafundishwa kuharibu amani ya watu wengine.
Sheikh Mohamed Magwila aliyeongoza sala katika Uwanja wa Samora mjini Iringa, alitaka Waislamu kudumu katika yale waliyojifunza wakati wa mfungo wa Ramadhani kuwa ndiyo kipimo cha mabadiliko.
“Sisi viongozi wa dini tunashirikiana na waumini wote kuiombea amani nchi yetu na katika suala la mchakato wa Katiba Mpya tunataka  maslahi ya umma yazingatiwe,” alisema.
Alisema siyo jambo jema kwa wahusika, hususan viongozi wanaoshughulikia jambo hilo kujikita katika kutetea ama masilahi ya kundi fulani au ya watu fulani katika jamii bali masilahi ya umma.
Mkoani Dodoma, Sheikh wa mkoa huo, Mustapha Shaaban aliwataka Waislamu nchini kuwaombea wajumbe wa Bunge la Katiba ili waweze kuelewana na kuliletea taifa Katiba bora yenye masilahi kwa Watanzania wote.
“Tuwaombee wajumbe wa Bunge la Katiba wawe na mshikamano utakaoliwezesha taifa letu kupata Katiba nzuri itakayotupeleka miaka mingine hamsini mbele,” alisema Sheikh Shaaban.
Aidha, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuweka kando masilahi yao binafsi, ushabiki wa vyama pamoja na taasisi zao ili waweze kulipatia taifa Katiba bora ambayo itakidhi mahitaji ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa na kitamaduni.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Imamu Kiongozi wa Msikiti Mkuu wa mkoa huo, Ustaadhi Thabiti Haji Tarimo aliwataka waumini hao kuendeleza mafunzo na matendo yote mazuri waliyoyapata wakati wa Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani.
Ustaadhi Tarimo alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kuendeleza ukarimu, upendo, ushirikiano, utulivu na subira.
Mkoani Tanga, Imamu Mkuu wa msikiti wa Ibadhi, Mohammed Said ameitaka jamii kuitunza amani ya nchi pamoja na kusameheana na kwamba bila ya amani maendeleo hayawezi kupatikana.
Alisema ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi wa amani na kwamba yoyote atakayekuwa chanzo cha uvunjifu huo anapaswa kuwajibishwa ili kuwa fundisho kwa wengine.
Dk Bilali
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal akiwa jijini Dar es Salaam alitoa mwito kwa Watanzania kudumisha amani na upendo ili kuleta umoja na mshikamano.
Akitoa salamu zake za sikukuu mara baada ya swala ya Idd jana asubuhi, Dk Bilal alisema mafunzo ya upendo na umoja yaliyokuwa yakitolewa wakati wa mfungo wa Ramadhani yaendelee kubaki miongoni mwa Watanzania siku zote.
“Napenda niwaombe ndugu zangu tuzingatie sana amani kwa sababu kuna wenzetu wanaendelea kukumbwa na misukosuko lakini sisi mwenyezi Mungu ameendelea kutulinda,” alisema Dk Bilal.
Aliwataka wananchi wote waiombee amani na kuongeza mshikamano miongoni mwa jamii na ulimwengu kwa ujumla ili kizazi kijacho kikue kwa furaha.
Mkoani Ruvuma, Waislamu wameshauriwa kuendeleza upendo amani na mshikamano waliouonyesha wakati wa Ramadhani kwa kuacha chuki, ulipizaji visasi na watumie muda wao wote kutenda mema ili kuinusuru nchi isiingie  kwenye machafuko.
Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alitoa wito huo wakati alipopewa nafasi ya kuwasalimia waumini waliohudhuria sala ya Idd na  akisisitiza kwamba lazima waepuke kujiingiza katika machafuko badala yake waendelee kuelekezana na kukosoana kwa busara.
Imeandikwa na Nuzulack Dausen, Dar, Geofrey Nyang’oro, Iringa, Josephine Sanga, Moshi, Rachel Chibwete, Dodoma, Salim Mohammed, Tanga, Joyce Joliga, Songea.