Malaysia imetangaza kutoa mchango wa glavu milioni 20 kwa mataifa 5 yanayopambana na homa hatari ya Ebola
Serikali ya Malaysia imesema kuwa glavu hizo zitatolewa kwa wafanyakazi wa afya nchini Liberia , Sierra Leone, Guinea, Nigeria na DRC.
Upungufu wa glavu hizo umezua wasiwasi wa kuenea kwa virusi hivyo,kwa mujibu wa maafisa wa Afya.
Nchi hiyo inaongoza kwa kutengeza glavu kwa asilimia 60 ya glavu zote duniani.
"Malaysia inaweza kutoa mchango wake wa kipekee kukabiliana na Ebola kwa sababu nchi yetu ni moja ya nchi zinazotengeza glovu duniani, '' alisema waziri mkuu Najib Razak.
"tunatumai kuwa mchango wetu utasaidia kuzuia kuenea kwa Ebola na kuokoa maisha.''
Zaidi ya nusu ya vifo vinavyotokana na Ebola vimetokea Liberia tangu mlipuko wa ugonjwa huu.
Sierra Leone, Guinea na Liberia ni baadhi ya mataifa yaliyoathiriwa vibaya sana na ugonjwa huo ambao hadi kufikia sasa umewaua zaidi ya watu 2,400 mwaka huu.
Miongoni mwa makampuni ambayo yametoa mchango huo ni pamoja na Sime Darby, Kuala Lumpur Kepong, IOI Corporation Berhad na Top Glove.