Mkuu wa Idara ya Usalama nchini Marekani, aliyekuwa na jukumu la kumlinda Rais Barack Obama, amejiuzulu kufuatia matukio yenye kuhatarisha usalama wa taifa yaliyotokea.
Mkuu huyo wa usalama Julia Pierson alikabidhi barua ya kujiuzulu kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Jumatano.
Siku moja kabla, alikabiliana na maswali ya wajumbe wenye hasira kutoka Baraza la Congress juu ya udhaifu mkubwa wa usalama wa Ikulu ya Marekani

Habari za tukio lingine likimhusisha mtu mwenye silaha kuruhusiwa kuingia katika lifti moja na Bwana Obama kulizidisha kutolewa wito wa kumtaka mkuu wa usalama kujiuzulu.
"Leo, Julia Pierson, mkurugenzi wa usalama wa taifa wa Marekani, amenikabidhi barua ya kujiuzulu, na nimeikubali," Waziri wa Usalama wa Taifa Jeh Johnson aliandika katika taarifa.
"Nampongeza kwa utumishi wake wa miaka 30 katika idara ya usalama na taifa."