Rais Jakaya Kikwete akipokea Katiba Inayopendekezwa kutoka kwa Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta wakati wa hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma juzi. Katikati ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Dar es Salaam. 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema haitaendesha uchaguzi wa aina yoyote, wala kuitisha kura ya maoni hadi kazi ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura itakapokamilika.
Kauli ya NEC imekuja siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa na Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na kulitaja suala la uboreshaji wa daftari la hilo kama mambo matatu yanayoiweka kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo njiapanda.
Mambo mengine ni Sheria inayotaka kura hiyo ipigwe ndani ya siku 84 baada ya Katiba inayopendekezwa kuchapishwa na kufanyiwa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema jana kwamba kuendesha uchaguzi bila kuboresha daftari hilo ni kuongeza malalamiko kwa wananchi na wadau, hususan vyama vya siasa.
“Msimamo wetu (NEC) ni kuwa bila daftari kuboreshwa hatuko tayari kuendesha uchaguzi wowote na hata huo wa kura ya maoni,” alisema na kuongeza:
“Sasa tuna takriban vijana milioni 2.3 ambao wamefikisha umri wa kupiga kura ... lakini kuna watu waliokufa, vyote hivi vinatakiwa kuboreshwa kwanza na sisi Tume hatuko tayari, naomba muwaambie wananchi.”
Kuhusu hoja kwamba NEC itumie daftari lililopo kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika uchaguzi mdogo mara kwa mara pale mbunge anapofariki dunia, Jaji Lubuva alisema tume yake haitaki yajirudie malalamiko ambayo imeyapata kupitia uchaguzi wa aina hiyo.
“Katika Uchaguzi wa Kalenga, Arumeru Mashariki na Chalinze, tulilalamikiwa sana kuhusu matumizi ya daftari hili, hivyo kutokana na malalamiko hayo yaliyotoka kwa vyama vya siasa, hatutaki tena kupata mengine kama hayo, ndiyo maana nasema muwaambie wananchi kwamba hatutaendesha chaguzi zozote hadi pale tutakapoboresha daftari,” alisema Jaji Lubuva.
Kuhusu lini kazi ya kuboresha daftari hilo itaanza, Jaji Lubuva alisema: “Tunasubiri vifaa vifike na vitakapofika tu tutaanza mara moja.”
Kauli ya Rais Kikwete
Akizungumza juzi katika sherehe ya makabidhiano ya Katiba inayopendekezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Kikwete alielezea maeneo matatu yenye utata ambayo yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi ili kufanikisha hatua hiyo.
Alisema suala la kwanza ni ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ambayo inaonyesha mchakato wa kuandika upya Daftari la Wapiga Kura utakamilika Mei 2015.Alisema suala hilo litaingiliana na mchakato wa Kura ya Maoni ambayo inatakiwa ifanyike ndani ya siku 84 tangu siku ambayo Katiba inayopendekezwa ilikabidhiwa kwa Rais.
Alisema ili suala hilo lifanikiwe, ni lazima Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe marekebisho, jambo ambalo linaweza kushughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atatakiwa kupeleka muswada bungeni.
“Ikifika Mei inabaki miezi miwili au mitatu kabla ya Bunge kuvunjwa na hapo ndipo watu huanza kampeni za uchaguzi mkuu.
“Lakini wapo pia wanaopingana na NEC. Wao wanasema mbona akifariki mbunge uchaguzi hufanyika. Jambo hili ninawaachieni na pale ambapo litapatiwa ufumbuzi mtaelezwa.”
Alisema kutokana na kuwapo kwa utata huo, ni jambo gumu kwa Katiba Mpya kupatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa sababu ya utata wa masuala hayo matatu, huku akisisitiza jambo hilo kutazamwa ili kuona kama linaweza kupatiwa ufumbuzi.