Marekani imewapongeza wananchi wa Burkina Faso na viongozi wao kwa kutia saini mkataba utakao ongoza serikali ya mpito kuelekea serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.
"Tunampongeza Michel Kafando kwa kuapishwa kuwa rais wa mpito wa Burkina Faso
Tunampa moyo Bwana Kafando kuendeleza kasi iliyoanza wiki mbili zilizopita na kuwachagua watu watakaosaidia kuendesha serikali ya mpito ambao wamejitolea kujenga serikali ya kiraia na kidemokrasia.

Tunayataka majeshi ya Burkina Faso kuendelea na jukumu lao la msingi la kulinda mipaka ya Burkina Faso na usalama wa raia wake. Pia kwa serikali ya mpito jukumu la serikali ya kiraia ya mpito ni kuhakikisha maandalizi kabambe kwa ajili ya uchaguzi wa kitaifa utakaofanyika mwezi Novemba 2015 kama ilivyoanishwa katika katiba"imesema taarifa ya Ikulu ya Marekani".

Serikali ya mpito Burkina Faso

Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Burkina Faso Michel Kafando, ametajwa kuwa rais wa mpito nchini humo.
Jitihada zimekuwa zikiendelea nchini humo kumchagua kiongozi wa mpito kufuatia kuidhinishwa hapo jana na jeshi na viongozi wa mashirika ya kiraia kwa mpango wa mwaka mzima utakaohakikisha kufanyika uchaguzi.
Kafando alikuwa mmoja kati ya watu wanne ambao wangechukua wadhifa huo, wakiwemo waandishi wawili na msomi mmoja.
Viongozi wa mashirika ya kiraia na wawakilishi wa jeshi walishughulika hadi usiku katika mji wa Ouagadougou kuamua nani atachukua wadhifa huo wa rais wa mpito.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya mpito, ilikuwa ni lazima awe raia ambaye hatogombea katika uchaguzi huo.
Mwishowe walimchagua raia aliyependwa zaidi na jeshi, mwenye umri wa miaka 72 na waziri wa mambo ya nje wa zamani Michel Kafando, Sasa ni lazima amchague waziri mkuu ambaye anaweza kuwa raia au afisa wa jeshi kuongoza serikali ya watu 25 ya mpito.