Rais Barack Obama amelihotubia taifa kueleza mageuzi makubwa katika mfumo wa uhamiaji wa Marekani. Amesema atachukua hatua za kikatiba kutoa ruhusa ya muda kisheria kwa takriban wahamiaji haramu milioni tano. Obama amesema nchi hiyo ilijengwa kwa uhamiaji na ameshutumu wanachama wa Republican kwa kuzuia mageuzi hayo. Wanachama hao wametishia kuchukua hatua.
Amesema watakaohalalishwa watalazimika kulipa kodi na wasiwe na rekodi ya uhalifu. Hata hivyo amesema urejeshwaji makwao kwa watu wenye makosa utaharakishwa.
Bwana Obama ametangaza mpango wake, ambao anaupitisha bila baraza la Congress, katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni.

Kwa upande wao wajumbe wa Republican wamesema hatua ya Rais Obama inavuka mipaka yake na uhusiano na rais utaingia dosari
Kuna wahamiaji wasio halali wapatao milioni 11 nchini Marekani na mwaka huu watoto wanaovuka mpaka wamesababisha tatizo.
Rais Obama ameliambia taifa kuwa kile anachopendekeza sio msamaha
"Ninachokieleza ni uwajibikaji - akili ya kawaida, mtazamo wa kawaida," amesema.
"Kama unatimiza vigezo, unaweza kujitokeza na kuishi maisha ya kawaida ukiendana na sheria."
"Iwapo ni mhalifu utarejeshwa ulikotoka.Kama unapanga kuingia Marekani kinyume cha sheria, nafasi ya kukamatwa na kurejeshwa ulikotoka ni kubwa." anasema Rais Obama.
Rais Obama amesema mfumo mpya wa uhamiaji utawawezesha watu wanaoishi nchini Marekani kinyume cha sheria, kujulikana na kuchangia katika uchumi wa taifa kwa kuwa watakuwa huru kufanyakazi.
Kuamuru kufanyika kwa mageuzi hayo kumesababisha malalamiko ya hasira kwa wanachama wa Republicans ambao wanasema hatua hiyo ni kutolishirikisha baraza la Congress na kuendesha mambo kwa mfumo wa Kifalme. Baadhi wanasema hawatatoa ushirikiano katika maeneo mengine ya kisera, na wengine wamemtaka Bwana Obama ashitakiwe.
Rais Obama anasema anachukua hatua hiyo kwa sababu baraza la Congress mara kadha kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu limeshindwa kurekebisha mfumo wa uhamiaji ambao umeharibika.