MUSA MATEJA/Amani

MAAJABU yanadaiwa kujitokeza kwenye maziko ya aliyekuwa staa wa Bongo Fleva kutoka Kundi la Chamber Squad, Moses Bushagama ‘Mez B’, ambapo jeneza lililobeba mwili wake lilidaiwa kugoma kuingia kaburini huku Wana-chamber wenzake, Haji Malick ‘Noorah’ na Athumani Kabongo ‘Dark Master’ wakiwa hoi baada ya kuishiwa nguvu na kusababisha watu wataharuki na wengine kuingiza imani za kishirikina.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Moses Bushagama ‘Mez B likiandaliwa kwa ajili ya kuagwa.
Maziko ya staa huyo yalifanyika Februari 23, mwaka huu kwenye
Makaburi ya Wahanga wa Treni, Mailimbili mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wakazi kibao wa mji huo waliochanganyikana na wasanii wa Bongo Fleva kutoka jijini Dar, ambao wote walijitolea katika kuhakikisha wanashuhudia safari ya mwisho ya Mez B.
Kuhusu kaburi, ilidaiwa kwamba moja ya changamoto katika kuupumzisha mwili huo ni jeneza kugoma kuingia kaburini na kuwafanya wachimbaji kuongeza ukubwa (upana) wa shimo ambao ulisababisha usumbufu.
Shuhuda wa Amani alidai kwamba, siku ya maziko hayo kulitokea hali ya sintofahamu, hasa baada ya kufikisha mwili wa marehemu eneo la makaburi, hasa changamoto na taharuki ilikuja baada ya jeneza kubana walipotaka kuzika hivyo wakalazimika kuliweka pembeni na kuanza kuchimba upya.
Jeneza likipelekwa makaburini kwa ajili ya mazishi.
“Kweli tumeshangazwa sana na ishu ya jeneza kubana kuingia kaburini, ninaamini kabisa madai ya kishirikina maana kulikuwa na wataalam wa kuchimba na hao siku zote huwa hawakosei vipimo, cha kushangaza ni kuona siku hiyo jeneza likibana.
“Ukiachilia mbali hilo, pia kulikuwa na ishu ya kuishiwa nguvu kwa Noorah na Dark Master ambao muda mwingi walikuwa wakijisikia kizunguzungu,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumzia ishu hiyo, Dark Master alisema kwamba, wanamshukuru Mungu harakati za maziko zilifanikiwa, isipokuwa kulikuwa na changamoto za hapo na pale likiwemo suala la jeneza kushindwa kuingia kaburini hali iliyowalazimu kusimamisha shughuli hiyo kwa muda na kupanua zaidi kaburi.
Alisema ishu nyingine ilimpata yeye na Noorah ambapo muda mwingi walikuwa wakipatwa na kizunguzungu na kuishiwa nguvu, kiasi cha kupoteza fahamu jambo ambalo si la kawaida kwa upande wake.
Mfiwa akilia kwa simanzi kubwa.
“Kweli ishu ya jeneza kubana kuingia katika kaburi ilijitokeza, jambo ambalo hata mimi lilinishangaza sana maana si kawaida kwa wachimbaji wa makaburi kukosea kipimo, sijui hasa ilikuwaje maana kamati ilikuwa na watu wengi, kuhusu mimi kujisikia kizunguzungu ni kweli hali hiyo ilinitokea sana nilipokuwa makaburini na kwa kiasi kikubwa nilikuwa nikiishiwa nguvu na kupotenza fahamu kabisa.
“Suala la kuishiwa nguvu halikuishia kwangu tu bali hata Noorah naye lilimkumba sana, ingawa yeye alipata msaada wa kuwa karibu na watu kwa muda wote tofauti na mimi ambaye nilikuwa nikizidiwa sana nakaa pembeni na naamka mwenyewe, namshukuru sana Mungu tumeweza kumsitiri mwenzetu pamoja na changamoto zote ambazo zimejitokeza,” alisema Dark Master.
Mez B ambaye alizaliwa mwaka 1982 alifariki dunia Februari 20, mwaka huu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua kikuu kwa muda mrefu.