DSC_01311-1024x681 (1)
Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mh. Alexandre Lévêque akimkabidhi tuzo ya kwanza Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania-TAMWA,Bi. Valerie Msoka kwa kufanikisha kampeni dhidi ya ndoa za utotoni.(Picha zote kwa hisani ya mtandao wa hivisasa.co.tz).
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) Valerie Msoka, amekuwa mtu wa kwanza kutunukiwa tuzo ya CEFM Champion, na Ubalozi wa Canada nchini.
Katika sherehe fupi iliyofanyika Serena Hotel 24 Februari 2015, Balozi wa Canada nchini Bwana Alexandre Leveque alisema kuwa Valerie Msoka amekuwa mwanaharakati wa kwanza kutunikiwa tuzo hiyo na ubalozi wake kama ishara ya kukubali mchango wake kupiga vita ndoa za utotoni, za kulazimishwa na ukeketaji kwa watoto wa kike nchini.
“Watoto wa kike na wanawake wamevumilia machungu ya ndoa za utotoni na za kulazimishwa hivyo wanahitaji mtu wa kuwasemea: mtu ambae ataelezea taarifa zao zinakazosaidia kuwaweka watu pamoja na kuleta mabadiliko yenye tija,”amesema Balozi Lévêque. Valerie Msoka atakuwa mtetezi. Ninafuraha kumtangaza kuwa Mtetezi wa CEFM wa Ubalozi wa Canada nchini Tanzania.”
Valerie ametumia ujuzi wake kama mwanahabari aliyebobea, mwanaharakati na mpenda maendeleo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bila kujali litakalomtokea au kueleweka vibaya na jamii.
Ameandika taarifa zenye kuvuta hisia, huruma na kuhamasisha kasi ya mabadiliko Katika jamii na watunga sera,” alisema Balozi Leveque.
DSC_02031-1024x681
Wapili kutoka kushoto ni Balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Lévêque , Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA Valerie Msoka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe na wawakilishi mbalimbali kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa wa masuala ya wanawake, UNFPA na UN Women.
Watoto wa kike milioni 14 duniani huozeshwa kila siku katika umri mdogo chini ya 18 jambo ambalo ni kinyume cha haki za mtoto na ukiukwaji wa haki za binadamu. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ndoa za utotoni na mikoa husika ni Shinyanga, Tabora, Mara, Lindi, Mbeya na Morogoro.
Balozi Leveque ameahidi kuunga mkono jitihada zinazomlinda mtoto wa kike ili kuendeleza kampeni ya Zero Marriage kwa mkoa wa Mara iliyozindiliwa mwaka 2014 na aliyekuwa mke wa Hayati Rais wa Kizalendo wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela, Graca Machel.
Akitoa shukrani baada ya kupokea tuzo hiyo, Valerie Msoka alisema kuwa ndoa za utotoni za kulazimishwa na ukeketaji vyote vinaenda pamoja na ni wajibu wa wadau mbalimbali ikiwemo serikali na vyombo vya habari kuendeleza kutoa elimu, kufanya tafiti ili kuwa na rekodi inayofahamika kuhusu ukubwa wa tatizo, kufuatilia mwenendo na mafanikio ya kampeni mbalimbali na kuendeleza hamasa kwa jamii kwa nini ndoa za utotoni zikomeshwe.
“Tukitaka kufanikisha kampeni hii ni lazima tufanye kazi kwa pamoja na kwa moyo mmoja, kuelewa nani anafanya nini kwa kiwango gani. Serikali nayo bado tunaitegemea sana kwa hali na mali katika kubadilisha sera zinazomkandamiza mtoto wa kike kwa kuzingatia mabadiliko ya katiba mpya”, alisema Valerie.
DSC_01191-1024x681 (1)
Wadau mbambali wa masula ya wanawake na waandishi wa habari wakongwe (Ma-Veterans), kutoka kushoto ni Fatuma Aloo pamoja na Mama Rose Haji Mwalimu wakihsuhudia tukio hilo.
“Tuzo hii ni yetu wote, kama sio kwa ushirikiano wenu wadau wa maendeleo, vyombo vya habari ambavyo tumefanya kazi kwa karibu sana na jamii kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushikamana kuhakikisha kuwa hadhi ya mtoto wa kike inalindwa ipasavyo”.
Hii ni mara ya pili kwa kiongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kupata tuzo ya kutambulika. Mwaka 2010 Ubalozi wa Marekani ulimtunuku Mkurugenzi aliyemaliza muda wake Ananilea Nkya tuzo ya Mwanamke Jasiri kutokana na mchango wake wa kuendeleza usawa, fursa na haki kwa wanawake wa wasichana wa Kitanzania.
Akitoa nasaha zake kwa niaba ya serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia Bi Anna Maembe amempongeza Msoka kwa kazi nzuri na chama anachokiendesha kwa ujumla na kusema kwamba tuzo hii imetolewa wakati ambapo dunia na taifa kwa ujumla linatafakari matokeo ya Beijing +20 ambako Katika maazimio 20 yaliyoainishwa, Tanzania ilipendekeza kulifanyia kazi azimio moja ambalo ni la kumlinda mtoto wa kike.
Maembe amesema tuzo hii itatoa hamasa kwa wengine na itakuwa kielelezo cha serikali Katika jitihada za kutekeleza tamko la CEDAW linalolenga kumlinda mwanamke na mtoto wa kike.
DSC_01341-1024x681
Mmoja wa wafanyakazi wa Chama cha wanahabari wanawake Tanzania TAMWA akiwakilisha zawadi ya ua kwa Mkurugenzi wao Valerie Msoka baada ya kukabidhiwa tunzo ya umahiri na utambuzi wa kupinga ndoa za utotoni na Ukeketaji nchini Tanzania kutoka nchini Canada.
Amesema serikali itaendeleza jitihada hizo kwa kuhakikisha watoto wa kike hawaolewi katika umri mdogo kwa kulazimishwa kwa kujenga mazingira mazuri shuleni yatakayovutia watoto wa kike kubaki mashuleni, kuongeza hamasa za uelewa wa tatizo na kuhakikisha wale wote wanaohusika na kuwalazimisha watoto wa kike kuolewa Katika umri mdogo wanachukuliwa hatua za kisheria. Lakini pia kuharakisha kubadilisha sharia ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo haimlindi mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.
“Watoto 2 kati ya 5 hujikuta wako Katika mazingira ya kuozeshwa kwa nguvu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutokuwa na elimu ya kutosha, maisha duni vijijini, umaskini na mila na desturi potofu zinazoendelezwa na baadhi ya makabila na mahari”, amesema Maembe.
Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 39 ya watoto wa kike wenye elimu ya msingi wameolewa katika umri usiotarajiwa chini ya miaka 18 wakati wale wenye elimu ya kutosha wa mjini wameolewa baada ya kufikisha miaka 18.
DSC_02181-1024x681
Mkurugenzi wa mtendaji wa TAMWA akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Chama hicho.
Ndoa za utotoni ni pale mtoto wa kike anapoozeshwa kwa lazima akiwa katika umri chini ya miaka 18 na wakati mwingine yuko shuleni. Madhara yake ni makubwa kwa afya ya mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai wake na mtoto mwenzake, kukosa maendeleo kimaisha na kuendeleza utamaduni wa kuwa tegemezi na kudumaza fikra na kumfanya kuwa duni Katika taifa.
Katiba ya nchi inamlinda mtoto wa kike kwa kutambua kwamba mtoto ni yule ambaye huko chini ya miaka 18 na hana sifa za kupiga kura. Lakini wakati huo huo Sheria ya Ndoa 1971 inasema mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 16 anaweza kuoa na msichana mwenye miaka 14 anaweza kuolewa kwa ridhaa ya wazazi.
Sheria hizi mbili zinakinzana na hivyo hazimlindi mtoto wa kike moja kwa moja. “Tutahakikisha kwamba sheria ya ndoa inafanyiwa marekebisho ili iende pamoja na Katiba ya nchi, jitihada zinaendelea kwa kuungana na wanaharakati wote nchini kuleta mabadiliko hasa baada ya kuzindua kampeni ya “Ukanda Huru wa Ndoa za Utotoni” (Child Marriage Free Zone) na Graca Machel.
Tuzo ya CEFM Champion ilishuhudiwa na wadau mbalimbali kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa kuchangia maendeleo, Umoja wa Kimataifa, waandishi wa habari na wanajamii.