Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuangalia ofisi ya (CUF) jimbo la Dimani iliyochomwa moto na watu wasiojulikana hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea Ofisi ya (CUF) jimbo la Dimani kuangalia uharibifu uliofanywa baada ya ofisi hiyo kuchomwa moto na watu wasiojulikana hivi karibuni. (picha na Salmin Said, OMKR)

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwajua watu waliohusika kuchoma moto ofisi za chama hicho jimbo la Dimani na baadaye wafikishwe mbele ya mkono wa sheria.
Maalim Seif amesema hayo wakati alipotembelea ofisi hizo zilizoteketezwa kabisa kwa moto, tukio lililofanywa na watu wasiojuilikana juzi usiku, huko katika eneo la Kisauni Wilaya ya Magharibi Unguja.
Katibu Mkuu wa CUF amesema tukio hilo ni la kusikitisha lililolengwa kuchafua hali ya amani na utulivu iliyopo Zanzibar, baada ya kufikiwa maridhiano ya kisiasa yaliyosababisha wananchi kuishi kwa amani.“Polisi hili ni tukio bay asana na hili sio la kwanza, kama mtawaachia watu hawa waendelee kufanya haya wataipeleka nchi hii pabaya”, amesema Maalim Seif alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea eneo hilo.
Aliwataka Polisi katika kufanya kazi yao kwa weledi na wasiingize mitazamo ya kisiasa hata kama kitendo hicho kimefanyiwa CUF, bali walichukulie ni tukio la kihalifu lililopangwa linalohitaji kufanyiwa kazi kwa kina.
Aidha, aliwataka wananchi hasa wanachama na wafuasi wa CUF wawe watulivu na wala wasilipike kisasi kwa sababu kitendo cha kulipa kisasi kitawafanya nao wanachangia vitendo vya kihalifu.

“Tunawaomba wanachama wa CUF wawe watulivu katika kipindi hichi na kamwe wasichokozeke kulipiza kisasi, wakifanya hivyo nao watakuwa wanachangia matukio ya kihalifu”, alionya Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amesema matukio ya kuchomeana moto ofisi na kushushwa bendera za vyama yameshapitwa na wakati Zanzibar yalijitokeza katika miaka ya 1990 hadi 2005 na yalikomeshwa baada ya maridhiano ya kisiasa, hivyo hayapaswi tena kukaribishwa Zanzibar.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ameitaka Kamati Tendaji ya chama hicho ibuni njia za kulijenga haraka jengo hilo la ofisi ya jimbo la Dimani katika eneo hilo hilo, ili iweze kutumiwa na wanachama wa eneo hilo.
Mapema akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa CUF, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani alisema mashuhuda wa tukio hilo walisema watu wasiojuilikana walifika katika ofisi hizo majira ya saa nane usiku wakiwa na gari  na waliposhuka waliingiza matairi ya gari ndani ya ofisi na baadaye kuilipua.
Bimani alimweza Maalim Seif kuwa kiasi cha shilingi milioni 135 zimepotea kufuatia hujuma hiyo.