Morogoro.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) milipuko hatari aina ya 'water explosive gel' iliyokamatwa jana usiku kutoka kwa watuhumiwa 10 waliokuwa wamehifadhiwa ndani ya msikiti wa Sunni uliopo tarafa ya Kidatu, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja anayesadikiwa kuhusiana na watu hao waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kumjeruhi kwa panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo limetokea jana (Aprili 14) majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.Kamanda Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri wake haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa kuwa wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua kufatilia nyendo zao.

Kamanda akionesha vilipuzi

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata askari huyo eneo la shingoni.

Askari mwingine mwenye namba E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo, ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka.”
Alisema polisi walendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.

Baadhi ya vifaa vilivyokamatwa msikitini na polisi ambapo watu 10 wanashikiliwa na jeshi hilo mjini Morogoro.

Kamanda huyo alitaja vitu vilivyokutwa katika mabegi yaliyokuwa ndani ya msikiti huo ni pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia, bisibisi, vinyago vya kuziba uso (masks), nguo za jeshi, misumeno ya chuma na spana.