INATISHA! Huku Wabongo wengi wakiendelea kukimbilia Afrika Kusini (Sauzi) kwa kigezo cha kutafuta maisha mazuri, imethibitika kwamba hali ya amani nchini humo si salama.

Wahamiaji wakionekana kujiokoa pamoja na watoto wao.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kutoka nchini humo, Wabongo wengi na wageni wengine kutoka nchi tofautitofauti Afrika kama Zimbabwe, Botswana, Namibia na nchi nyingine wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili na hata kuuawa na wenyeji wa nchi hiyo wakidai wanawakosesha ajira.
“Jamani hali inatisha sana huku, wageni tunauawa sana, wengine wanachomwa moto na kuchomwa visu hadharani, hakuna amani tena,” alisema Mbongo mmoja anayeishi nchini humo.Chanzo kiliendelea kudadavua kwamba Waafrika Kusini wanachukizwa na wageni hao kwani wamekuwa wakipokea ajira kutoka kwa matajiri kiasi kwamba wao wameonekana hawafai kwani wengi hawataki kazi ngumu tofauti na ilivyo kwa wageni ambao hupiga kazi yoyote bila kujali ugumu wa kazi.
Wahamiaji wakiwa kwenye hifadhi baada ya kukimbia machafuko.
Imeelezwa kuwa usalama wa wageni nchini humo umekuwa mdogo mno kiasi kwamba wengine wamekuwa wakijificha ndani kwa wiki nzima pasipo kutoka nje kwa kuhofia kuuawa na wenyeji ambao wamekuwa wakirandaranda mitaani kuwatafuta wageni ili wawadhuru.
“Sijatoka nyumbani wiki nzima, nipo nimejifungia tu, hata kwenda kununua chakula inakuwa ngumu sana, jamani, chondechonde waambie Watanzania wasikimbilie huku, hali inatisha sana,” kilisema chanzo chetu.
Mara baada ya kusambaa kwa taarifa za mauaji yanayoendelea kutokea Afrika Kusini, Watanzania wengi wameonekana kukasirishwa na kitendo hicho hivyo kukemea vikali mauaji hayo.
“Hii siyo fair kabisa, sifurahii kuona ndugu zetu wakiuawa huko, naomba warudi nyumbani na hata sisi tuliokuwa hapa nyumbani tutulie tu kwani maisha popote pale,” alisema kijana mmoja aishiye Manzese Midizini.