Baadhi ya wasichana wa Uingereza waliojiunga na wapiganaji wa IS nchini Syria
Wasichana wawili walio marafiki wakubwa wametoweka kutoka nyumbani kwao mjini Nairobi nchini Kenya na wanashukiwa kusafiri nchini Syria ili kujiunga na kundi la wapiganaji wa ISIS.
Waliondoka nyumbani kwao wakati tofauti wakidai kwamba walikuwa wakielekea katika shule moja ya kiislamu lakini sasa wametoweka.

Ndugu na jamaa za wasichana hao wanasema kuwa walipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa wasichana hao akisema kuwa wako nchini Syria.
Kulingana na mwandishi wa BBC Joseph Odhiambo,Salwa Abdalla na Tawfiqa Dahir walitoa sababu tofauti za kuondoka nyumbani.
Salwa ambaye ni mwanafunzi katika shule ya Nairobi Muslim alisema kuwa alikuwa akirudi shuleni humo huku Tawfiqa naye akiondoka nyumbani kwa madai kwamba alikuwa anaelekea kuwachukua binamu zake wawili kutoka shule hiyo.
Mama ya mmoja wa wasichana hao alionyesha ujumbe kutoka vyombo vya habari unaoaminika kutoka kwa mwanawe,akiwaambia kwamba yuko nchini Syria akijaribu kuanza maisha.
Mamazao wasichana hao wawili waliripoti kupotea kwao kwa polisi,wakihofia kwamba watoto wao huenda walisafiri kujiunga na kundi la Islamic State.
Mamaake Twafiqa alimwelezea mwandishi huyu katika simu kwamba yeye anaishi Mandera kazkazini Magharibi mwa Kenya huku yeye akiishi mjini Nairobi ambapo anasoma.
Amesema kuwa wakati mwanawe alipokuwa hapatikani,alilazimika kusafiri hadi Nairobi mara moja ili kujiunga na utafutaji wake.
Amesema ''binamu yake amepokea ujumbe 27 zinazoaminika kutoka kwake. Pia wamezungumza naye kwa njia ya simu na kudai kwamba yupo nchini Syria. Lakini sijui ukweli''.
Maafisa wa polisi hatahivyo wamekataa kulizungumzia swala hilo.
Ripoti za watu kutoka barani Afrika kuondoka ili kujiunga na ISIS ni nadra.