Sudani kusini ni taifa changa zaidi duniani ambalo maendeleo yake yanafifia kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
Vikosi vya Usalama nchini Sudani Kusini vimefunga kituo cha redio iliyokuwa ikiunga mkono mpango wa kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.
Mamlaka ya nchi hiyo, imekilazimisha kituo cha radio cha Free Voice South Sudan kinachoungwa mkono na Marekani kutorusha matangazo yake siku ya Jumanne, siku moja tu baada ya kulifungia gazeti la The Citizen.
Wapatanishi wa kimataifa wamewapa rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar mpaka katikati ya mwezi Agosti kusaini makubaliano ya amani.
Kwa upande wake, rais Obama amewatuhumu viongozi hao wawili kwa kile alichokiita kusambaratisha matumaini ya taifa changa zaidi duniani.
Mpaka sasa maelfu ya vijana wameuawa na takriban watu milioni moja na nusu wamekimbia makazi yao tangu mgogoro huo ulipoanza yapata miaka miwili iliyopita.