MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, amewataka Watanzania kuwa makini wasije kudanganywa na matapeli wa kisiasa watakaokuja na ahadi za uongo.
Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana, Dk Magufuli alisema matapeli hao watakuja na ahadi nyingi, akawataka wananchi wawasikilize na kuwapima kwa kauli na sifa zao kwa kuwa kuahidi ni rahisi kuliko kutekeleza.

“Tusije tukadanganywa na matapeli wa kisiasa, wakinamama mnafahamu matapeli wa mjini walivyo na maneno matamu. Maendeleo ni changamoto na yataletwa na sisi Wanamtwara,” alisema.
Miongoni mwa matazamio ya Dk Magufuli ya Serikali atakayoiongoza kama akichaguliwa kuwa rais, ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mtwara kupitia Songea mpaka Mbambabay, baada ya kuboresha Bandari ya Mtwara na kuwa ya kisasa kama ya Dar es Salaam.
Alisema bandari itaboreshwa ili pia iongeze ajira kwa wakazi wa mji huo huku mizigo ya nchi za Zambia na Malawi, ikipitia mkoani humo.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza, itajielekeza zaidi katika kukuza uchumi kwa watu. Akizungumza katika mikutano mikubwa na midogo katika wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini kuhusu zao la korosho, Dk Magufuli alisema katika uongozi wake, lazima korosho ilete uchumi mzuri kwa wakazi wa Mtwara.
“Mimi shahada yangu ya tatu (PHD) nimesomea korosho. Hakuna anayeweza kunidanganya. Korosho siyo tu tunda la ndani, bali hata ganda ni uchumi kwa kuwa linatengeneza gundi na dawa ya kuzuia kutu,” alisema Dk Magufuli.
Alisema korosho ya Tanzania ni tofauti na korosho nyingine duniani, kwa kuwa yenyewe huanza kuvunwa wakati maeneo mengine duniani wamemaliza kuvuna.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, katika uongozi wake hataruhusu korosho kuuzwa ghafi nje ya nchi, bali Serikali itahakikisha kunajengwa viwanda vitakavyotumia malighafi ya korosho ili zao hilo lipande bei.
Kuhusu tatizo la stakabadhi ghalani ambalo limekuwa likilalamikiwa na wakulima, Dk Magufuli alisema wamuachie yeye atahakikisha kero ya mfumo huo inaondoshwa na wakulima hawadhulumiwi haki yao.
Akiwa Mtwara vijijini, alisema Tanzania imegundua gesi mkoani Mtwara, hivyo akaahidi kuhakikisha gesi hiyo inaanza kunufaisha wakazi wa Mtwara kabla ya kunufaisha wananchi wa mikoa mingine.
Katika hilo, alisema atasimamia ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, ili vitoe ajira kwa vijana wa Mtwara, ambao watakuwa wamesoma katika shule mbalimbali, ambazo kuanzia mwakani kutoka shule ya awali mpaka kidato cha nne, itakuwa bure.
Awali kabla ya kutoa ahadi hizo na zingine nyingi katika sekta mbalimbali, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, William Lukuvi, alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee wa urais kwa sasa aliyetembea kwa barabara umbali mrefu.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Dk Magufuli ambaye amemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kampeni katika mikoa saba, kutoka Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma na kumalizia Mtwara jana kwa barabara, pia ndiye mgombeapekee wa urais aliyechaguliwa katika mchakato bora na ulio wazi.
“Wako wanaodai kulikuwa na mizengwe wakati wa kumpata mgombea wa CCM. Ngoja niwaambie, walikuwa wagombea 38, tukachuja mpaka wakabakia watano na Magufuli akiwepo. Tukachuja tena katika mchakato wa wazi mpaka watatu na Magufuli akawepo na wakati wa kumpata mmoja, ambaye ndiye Magufuli, mchakato ulirushwa moja kwa moja na televisheni nchi nzima.“Sasa tuwaulize wenzetu walikuwa wangapi na walimpataje huyo mgombea wao, mbona hatukuwaona?” Alihoji na kuongeza kuwa Dk Magufuli ni mgombea safi na hata marafiki zake si wa hovyo na watu wa hovyo wanaogopa kumkaribia.
Lukuvi alisema kama Watanzania wanataka bora rais, basi huyo si Dk Magufuli, lakini kama wanataka rais bora, basi kati ya wagombea wote wa urais, hakuna aliye bora kama Dk Magufuli.