Rais Dk. Ali Mohamed Shein.
KWANZA tumsifu Mungu kwa kuendelea kuwapa moyo wa amani Watanzania, hili ni jambo muhimu kuliko kitu chochote hapa nchini.
Nianze kwa kusema kwamba kwa namna ambavyo vyama vya siasa vinaendesha mambo yao na demokrasia iliyomo ndani ya vyama hivyo ndivyo ambavyo vitaendesha nchi ikiwa mgombea urais atachaguliwa na wananchi kuongoza nchi.

Tusisahau pia kwamba madaraka hulevya; na hata kiongozi mzuri wakati hayupo kwenye madaraka hufaa kuchungwa anapokuwa kwenye madaraka, hivyo basi umakini mkubwa unahitajika kwa wananchi kuwachambua wagombea urais ili hatimaye kuchagua mtu makini.
Zanzibar vyama vimeteua wagombea, lakini wenye nguvu ni Rais Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamadi ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF).
Tanzania Bara vyama vyenye nguvu navyo vimeteua wagombea, CCM mpeperusha bendera yao ni Dk. John Pombe Magufuli na Ukawa chini ya Chadema ni Edward Ngoyai Lowassa ambao kwa kweli vyama hivyo vina nguvu sana.
Tunajua kuwa kwenye nafasi za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na madiwani wapinzani Ukawa wameachiana majimbo kuona nani anakubalika sehemu husika.

‘Mwongozo wa TANU’ (chama kilicholeta uhuru) unasema kwamba ‘kiongozi ni mtu aliyetosheka’ kwa hiyo CCM imemuibua Dk. Magufuli ambaye ni mchapakazi kwelikweli na ametosheka, hana doa la ufisadi.
Tunavyojua Watanzania ni kwamba mgombea wa chama hupatikana baada ya kuthibitishwa na vikao vya maamuzi vinavyohusika vya chama ndipo baadaye huwa ni mgombea rasmi wa chama, hivyo Dk. Magufuli ndani ya CCM ndiye chaguo la chama na inapaswa makundi kuyafuta ikiwa CCM watataka ushindi wa kishindo.
Nasema hivyo kwa sababu CCM inaonesha kujiamini kwamba itashinda kiti cha urais wa Jamhuri kwa kishindo. Huku si kuvikatisha tamaa vyama vya upinzani, bali kama usemi unavyosema, mtu huvuna anachopanda.
Wakati bado upo muda wa vyama vya upinzani kujinadi hivyo kutoa ushindani mkubwa kwa CCM, Ukawa wanapaswa kushikamana kwa sababu hakuna siri kwamba chama tawala kina mizizi mikubwa, hasa vijijini na nasema hivyo kwa sababu huo ndiyo ukweli wenyewe.

Nitoe ushauri kwa yeyote atakayeshinda kiti cha urais wa Jamhuri kwamba kuna mambo matatu ningeomba ayafikirie. Kwanza, ni amani, utulivu na umoja wa kitaifa. Hakuwezi kuwepo amani baina ya aliyeshiba na mwenye njaa;
akutokuwa na utulivu baina ya watoto wa wachache wanaopata elimu nzuri na wale wa wengi wanaopata elimu duni.
Jambo la pili rais ajaye ni lazima aweke kipaumbele kuhusu mshikamano na umoja wa kitaifa, ajue kwamba ikiwa hakuna utulivu hasa Zanzibar tusifikirie kwamba Tanzania itatajwa duniani kwamba ni kisiwa cha amani. 
Tatu, sera zetu za kiuchumi na kijamii ingefaa zikaangaliwa upya. Haifai hata kidogo kujenga taifa la ombaomba na tegemezi, yaani Bajeti ya Taifa inabebwa na wafadhili, hii haifai.

Katika taifa kama letu haina maana kusema kwamba serikali inajitoa kwenye hili na lile na wajibu wake pekee ni ulinzi na usalama tu, hapana, naamini serikali ina njia nyingi ya kulifanya taifa kujitegemea tukijikita kwenye kilimo cha kisasa, sekta ya madini ikisimamiwa vizuri, utalii, bandari tutaweza kujitegemea.
Hakuna nchi iliyoendelea bila ya dola kusimamia kikamilifu mwenendo wa uchumi, kuendeleza sera za kijamii na kulinda maadili na utamaduni wake.Nne, elimu ipewe kipaumbele, rais ajaye ni lazima atilie mkazo mkubwa katika kukuza elimu kwenye viwango vyote; rasilimali nyingi ziwekwe kwenye sekta ya elimu; na kila kijiji, mtaa na wilaya zihamasishwe kutoa elimu bora na siyo bora elimu.
Kuna haja kwa sasa kuona uongozi wa aina mpya ya Dk. Magufuli ambaye hupenda vitendo kuliko maneno. Nathibitisha kuwa Magufuli siyo mtu wa kushinda ofisini. Yeye hutoa maagizo na kufuatilia na kiongozi wa aina hii ndiye anayefaa kuongoza Tanzania kwa sasa.
CCM ina taratibu za kufuatwa katika kubadilishana uongozi na siyo kama tunavyoona sasa kwa baadhi ya vyama ambavyo humchukua mtu aliyejiunga jana bila utaratibu na matokeo yake baadhi ya wanachama kususa au kujiondoa katika uongozi na kusababisha chama kuyumba.
Ushauri wangu wa mwisho kwa Watanzania ni kwamba kila mpiga kura awe makini wakati wa kuchagua, hasa nafasi ya urais, kwamba huyu ninayemchagua ataweza kuongoza taifa hili kwa haki bila kulipiza kisasi?
Nitoe onyo, mshindani yeyote anayetumia fedha, huyo siyo mwenzetu na hafai kuwa kiongozi wetu kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais, huyo asichaguliwe, hivyo tuwe makini kuchagua rais wa awamu ya tano