MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema endapo uchaguzi utafanyika leo, atashinda kwa asilimia 80, lakini akasema anachokifanya sasa ni kupita kwa wananchi ili kuongeza idadi ya kura kufikia asilimia zaidi ya 90.
Aidha, amesema dhamira yake, pamoja na kuwa lengo la kuifanyia nchi mambo mengi, anataka kuhakikisha anarejesha hadhi ya Jiji la kitalii la Arusha ambalo katika miaka ya hivi karibuni limekuwa likikabiliwa na maandamano ya mara kwa mara, lakini pia ameeleza kuguswa na kuzorota kwa hadhi ya wilaya la Monduli, aliyoiita anaiheshimu mno kutokana na kuwahi kutoka Waziri Mkuu mwadilifu na mchapakazi, Hayati Edward Moringe Sokoine.

Kutokana na hayo, amewaomba wakazi wa Jimbo la Monduli, Longido na Arusha kutopoteza kura zao kwa vile endapo watamchagua mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa watapoteza kura zao.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amewapa pole wakazi wa Mto wa Mbu na Monduli kwa jimbo lao kukabiliwa na kero nyingi za wananchi, akisema wapo wagombea wa CCM ambao huwa wabaya na ambao hawajali matatizo ya wananchi wanaowachagua.
Aliyasema hayo alipohutubia mikutano ya hadhara katika miji mbalimbali ya mkoa wa Arusha, ukiwamo mkubwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katikati ya Jiji la Arusha. “ Naomba mnichague kwa kura nyingi. Nitafanya kazi kama Sokoine aliyewatumikia Watanzania kwa bidii na moyo wake wote.
Sokoine alichukia ufisadi na aliupiga vita,” alisema Magufuli. Kuhusu uhakika wa ushindi, Dk Magufuli alisema; “Naomba niwaombe wananchi wa Monduli na Arusha, mnichague mimi, maana ni lazima nitakuwa Rais, hivyo ni vyema mkanipa hizo kura zenu ili zisipotee.
“Endapo uchaguzi utafanyika leo, nitashinda kwa zaidi ya asilimia 80, ninachofanya sasa ni kupita ili kuomba kura zaidi ili zifike kura asilimia zaidi ya 90,” alisema Dk Magufuli. Mgombea huyo wa CCM aliwahakikishia wakazi wa Arusha kwamba endapo atachaguliwa kuwa rais, atafanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa bila kuwabagua wananchi kwa utofauti wao wa vyama, dini, makabila wala maeneo wanayotoka.
Aidha, aliwapa pole wakazi wa Jimbo la Monduli katika Mji wa Mto wa Mbu, waliojitokeza na kueleza kilio chao kwa kukosa huduma muhimu za jamii ikiwemo maji, masoko, benki, mabwawa ya maji kwa mifugo na ofisi ya malipo ya umeme, hatua inayowafanya kusafiri hadi wilaya jirani ya Karatu kupata huduma hizo.
Mmoja wa wananchi hao, Donosia Thomas kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja wilayani Monduli, alimwambia Dk Magufuli kuwa mbali ya matatizo hayo wananchi wanalazimishwa kuchangia debe la mahindi, kilo tano za maharage, kilo moja ya chumvi, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi na kwamba wazazi wanaposhindwa, watoto wao hufukuzwa shule.
Alisema umasikini uliopo Monduli unatokana na kuwepo kwa wanaCCM wabaya ambao huchaguliwa na wananchi bila kujua kuwa wapo wanaCCM wabaya zaidi na ambao hawapaswi kuchaguliwa kwa vile hawana uchungu na matatizo ya wananchi.
Dk Magufuli alisema ili kumuenzi Sokoine akiwa Rais atafufua upya mabwawa ya maji kwa mifugo ambayo yalikufa baada ya kifo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani kilichotokana na ajali ya gari Aprili 12, 1984 mkoani Morogoro.
Kutaifisha viwanda Dk Magufuli anayesifika pia kwa uchapakazi, ameongeza kuwa akichaguliwa kushika wadhifa huo, atataifisha viwanda vyote ambavyo wamiliki wake wameshindwa kuviendesha.
Aliahidi pia kuwachukulia hatua kali watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutokana kukatikakatika kwa umeme na kwamba anafanya utafiti kubaini kama kitendo hicho ni hujuma dhidi yake na ikibainika hivyo atawafukuza mara moja watendaji wa shirika hilo baada ya kuapishwa.
Aliwataka Mawaziri wanaosimamia sekta ya umeme akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye kwa sasa anaomba kura za ubunge katika Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma, kufuatilia kujua chanzo cha kukatikakatika kwa umeme haraka.
Mkutano wa Arusha Akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Arusha waliohudhuria mkutano wa kampeni wa CCM jana, Dk Magufuli alisema wamiliki wa viwanda waliovichukua viwanda hivyo baada ya kubinafsishwa wahakikishe kuwa viwanda hivyo vinafanya kazi kabla ya kuapishwa.
Alisema serikali yake kamwe haitakubali kuona wananchi wakikosa ajira wakati vipo viwanda vilibinafsishwa na waliovichukua wamevitelekeza na alitolea mfano viwanda vya General Tyre na Kilitex kuwa wamiliki waanze kuzalisha haraka ili kuwapatia wananchi ajira.
“Siwezi kukubali katika uongozi wangu, watu wachache wa juu wafaidi kutokana na ufisadi huku wananchi wengi wakiwa masikini, nawaahidi kuwa serikali yangu itakuwa ni kazi tu,” alisema Dk Magufuli.
Alisema atakapoingia madarakani ataufanya mji wa Arusha kuwa kitovu cha utalii na ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki, hatua aliyosema itachangia maendeleo ya haraka kwa mji huo huku akisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita sifa ya Arusha imetetereka kutokana na fujo za mara kwa mara.
“Nawahakikishia viongozi wenzangu wa Afrika Mashariki wasiwe na wasiwasi na Magufuli, tutaendeleza ushirikiano ulioanzishwa na watangulizi wangu ili kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa bora zaidi na uchumi wa mataifa yote unaimarika,” alisema.
Alitoa ahadi kwa wafanyakazi kushusha chini makato ya mshahara kutoka asilimia 11 ya sasa, huku akisema kazi hiyo imeshaanza kufanywa kutokana na kuwepo kwa Tume inayoendelea kutathmini malipo ya mishahara kwa wafanyakazi ili Watanzania wote wapate mishahara mizuri.
“Tutafuatilia hili la mishahara kwa karibu sana, maana asilimia 99.999 ya wafanyakazi wanafanya kazi nzuri na hawapokei rushwa lakini wapo wachache sana ambao ni mabingwa wa rushwa na hao naomba wajirekebishe haraka kabla sijaingia madarakani,” alisema.
Aliahidi pia kusimamia ili kubadilishwa kwa sheria ili wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu na kada nyingine wasitakiwe kuwa na uzoefu wa miaka mingi kama kigezo cha kupata kazi serikalini na kwingineko akisema hatua hiyo imekuwa inawafanya Watanzania kukosa kazi na wageni kunufaika.
Alisema pia ataboresha miundombinu ya mji wa Arusha ikiwemo maji, barabara za lami, ajira kwa vijana huku akisema suala la ajira kwa vijana halihitaji ahadi za matumaini bali hatua madhubuti ambazo alisema serikali yake ndiyo yenye majibu kwa mageuzi katika soko la ajira nchini.
Kuhusu sekta ya mifugo aliahidi kuanzishwa kwa viwanda vya nyama ili kuwezesha wafugaji kupata soko la mifugo yao na kuongeza kipato chao, huku akisema Tanzania chini ya utawala wake itakuwa na kiwanda cha ngozi Arusha kitakachozalisha ajira.
Alisema uwepo wa kiwanda hicho kutafanya kuzaliwa kwa viwanda vya nyama, viatu, mikanda, maziwa na vinginevyo na hivyo kufanya bidhaa hizo kuachwa kuagizwa kutoka nje hatua ambayo pia itakuza uchumi, kipato cha wananchi na pia kuongeza pato la serikali.
Kinana na posho Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema mara baada ya kuingia madarakani, CCM itamuomba Magufuli kufuta posho za maofisa serikalini, na kuondoa kero kwa wananchi za uzembe na ufisadi, akitolea mfano suala la mgawo wa umeme aliosema umekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Kinana alimuomba Magufuli pamoja na kutaifisha viwanda vya mijini na vijijini, ambavyo wamiliki wake hawaviendeshi baada ya serikali kuvibinafsisha, pia akomeshe mara moja vikao na posho serikalini kwa kufuta vitu hivyo na kuwabana watendaji kufanya kazi, tofauti na ilivyo sasa.
“Nchi hii sasa imekuwa ya vikao. Vikao ni vingi sana. Watumishi wengi wanapoteza muda mwingi na pesa katika vikao,” alisema Kinana na kumwomba Magufuli atakapochaguliwa kukomesha tabia hiyo.
Kinana alisema kuna tabia ya urasimu katika ofisi nyingi, ambapo wananchi wanaotaka huduma katika ofisi hizo, wamekuwa wakizungushwa bila kuhudumiwa na kupewa kauli za ‘njoo kesho’. Aliomba Magufuli kuondoa urasimu huo.
Kuhusu mabadiliko, Kinana alisema wapo watu wanaodanganya kuwa wataleta mabadiliko nchini. Alisema mabadiliko ya kweli yataletwa na Dk Magufuli na CCM. “Kuna watu wanazungumza juu ya mabadiliko. Tunaomba wananchi mtambue kuwa mabadiliko bora na ya kweli yataletwa na CCM na Magufuli.
Serikali ya CCM ya Rais Jakaya Kikwete imeleta mabadiliko mengi ya kiuchumi na kijamii na mabadiliko bora na ya kweli, yataendelea kuletwa na Magufuli,” alisema Kinana na kuomba Watanzania kumpigia kura nyingi Magufuli na wagombea ubunge na udiwani wa CCM.