04
 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na viongozi wa ulinzi na usalama wilaya ya Kinondoni walipotembelea na kujionea maeneo yaliyojengwa kuzunguka matenki ya maji Kimara mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam. Wa kwanza kulia ni Meneja wa Miundombinu Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi John Kirecha.
Na Eleuteri Mangi – MAELEZO
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ameuagiza uongozi wa  Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) kuandaa orodha ya wananchi waliojenga juu ya miundo mbinu ya maji na kuipeleka orodha hiyo ofisini kwake kwa hatua zaidi.
Akiongea na uongozi wa DAWASA mwishoni mwa wiki baada ya kuhitimisha ziara yake ya kujionea hatua zilizofikiwa kwenye mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulazaji wa bomba kuu la maji kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa tanki jipya la Kibamba na kukarabati matenki ya maji Kimara, Makonda alisema kuwa nia ya Serikali kuwapa huduma ya maji wananchi kwa wakati.
“Nataka kazi hii ya ujenzi wa mradi wa bomba la maji ukamilike kwa muda ulivyopangwa uweze kuwaondolea wananchi kero ya maji inayowasumbua, huduma ya maji ni ya muhimu sana kwa wakazi wa Dar es salaam, upatikanaji wake utasaidia kupunguza magonjwa mengi hasa ya milipuko ambayo ni hatari kwa afya wananchi wetu” alisema Makonda.
08
DC Makonda akiwa katika eneo la tukio hilo 
Agizo la Mkuu huyo wa Wilaya linafuatia kuwepo kwa vikwazo mbalimbali vinavyochelewesha mradi wa ujenzi wa bomba hilo kukamilika kwa wakati katika maeneo ya Kimara yalipo matangi ya maji ambapo makazi ya watu yamejengewa kuzunguka matangi hayo na kuhatarisha usalama wa maisha ya wakazi hao na usalama wa miundombinu ya maji.
Eneo lingine ambalo limekuwa kikwazo cha kukamilisha mradi huo ni Kibamba Luguruni ambapo mabomba ya mradi yamezuiliwa kwa kufungiwa na kuzungushiwa kwenye uzio na mkazi wa eneo hilo Bw. Enock E. Mwakassala.
Kwa mujibu wa DAWASA, mkazi huyo hana uhalali wa kumiliki eneo hilo maana amevamia eneo la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa sababu zake binafsi na hivyo kuchelewesha ujenzi wa mradi.
Aidha, Makonda ameuagiza uongozi wa DAWASA kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwaainisha watu wote waliojenga ndani ya hifadhi ya eneo la miundombinu ya shirika hilo ambalo limetoa sehemu ya hifdhi yake kwa lengo la kujenga na kulaza bomba jipya la kusambaza maji kutoka Mlandizi hadi Kimara yalipo matangi ya kusambazia maji ambayo yatawanufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
11
Baadhi ya vifaa katika ujenzi huo..
Kwa upande wake Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo kutoka DAWASA Christian Christopher amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Juu una jumla ya km 69 ambapo hadi sasa km 46 ujenzi wake tayari umekamilika na zimebakia km 23 ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari 2016.
Mhandisi Christian alisema kuwa mradi wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Juu unatekelewa na kampuni ya MEGHA kutoka nchini India inayoongozwa na Meneja wake Mohan Dendkri  chini ya makubaliano ya kandarasi Na. AE/033/2012-13/WC/25.
Vile vile Mhandisi Christian aliongeza kuwa kutoka eneo la Mlandizi ambalo ndiyo chanzo cha maji yanapotoka yatasafirishwa kwa bomba lenye kipenyo cha ukubwa mm 1200 hadi Kibamba ambapo linajengwa tangi la maji lenye uwezo wa ujazo wa lita milioni 10 kwa siku na baadaye maji hayo kusafirishwa hadi Kimara, kipenyo cha bomba la kutoka Kibamba hahi Kimara ni mm 1000 na kutoka Tanita hadi Kibamba bomba hilo lina kipenyo cha mm 900.
Wakazi wa jiji la Dar es salaa asilimia 25 wanategemea maji kutoka chanzo cha Ruvu Juu na asilimia 75 wanapata maji kutoka chanzo cha maji kutoka Ruvu Chini. Mtambo  wa  Ruvu  Juu  unahudumia  wakazi  wa  Mlandizi,  mji  wa  Kibaha na  maeneo  ya Kiluvya,  Mbezi,  Kimara,  Ubungo,  Tabata  na  Segerea.  Mtambo  wa  Ruvu Chini unahudumia maeneo ya Mji wa Bagamoyo, Bunju. Boko, Mbezi Beach, Kawe, Kinondoni, katikati  ya  Jiji,  Sinza,  Magomeni,  Buguruni,  Ilala  na  Keko.  Mtambo  wa  Mtoni  unahudumia maeneo  ya  Temeke,  Tandika,  Kurasini,  baadhi  ya  maeneo  ya  Keko  na  Mbagala.
05
06
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda na msafara wake wakiwa eneo linapojengwa tanki jipya la maji eneo la Kibamba ambalo litakuwa uwezo wa ujazo wa lita milioni 10 kwa siku na kujionea shughuli za ujenzi huo unavyoendelea wakati wa ziara yake mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.