WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu watambue jukumu walilonalo la kuwahudumia wananchi kutokana na majukumu ya ofisi hiyo yanayogusa maisha ya kila siku ya Watanzania.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa na pana sana na inahusika na shughuli za kila siku za Watanzania. Kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kukidhi matarajio yao,” alisema Majaliwa. Alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
kwenye mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Jana ndiyo aliripoti kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Ijumaa iliyopita kwenye Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. “Pamoja na kazi nyingine, tunayo majukumu makubwa ambayo ni udhibiti, usimamizi na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali humu serikalini.
Ninatarajia kupata mpango kazi kutoka kwa Mkuu wa kila idara na kila taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitakwenda pia ofisi za Tamisemi ili kuweka vipaumbele vyetu sawa,” alisema.
Aliwataka watumishi hao wawe tayari kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo imekuwa ikisisitizwa na Rais John Magufuli ili kumudu kasi ya utendaji kazi Serikalini ambayo anahimiza hivi sasa. Alisema ana imani kuwa watumishi hao watampa ushirikiano kama ambavyo walikuwa wakiutoa kwa mtangulizi wake, Mizengo Pinda ambaye amestaafu hivi karibuni.