CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) - Zanzibar kimesema mazungumzo yanayoendelea nchini yakiwahusisha viongozi wakuu wa kisiasa kamwe hayajazuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa. Alisema hawawezi kukwepa mazungumzo katika kukuza demokrasia kama ni sehemu ya kuimarisha amani na utulivu wa nchi.
Hata hivyo, alisema mazingira hayo kamwe hayawezi kuwa mbadala wa sheria zilizopo nchini ambapo kwa upande wa ZEC imetangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu na kutaka wananchi wajiandae kutangaziwa tarehe mpya ya Uchaguzi Mkuu.

Alisema tayari Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imetangaza kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25 kupitia Gazeti la Serikali na hivyo kuashiria kutoa nafasi kwa ZEC kufanya maandalizi ya uchaguzi mwingine.
Mapema, Vuai aliwataka wanaCCM Zanzibar kujiandaa na uchaguzi wa marudio na kuepukana na propaganda zinazotolewa na wapinzani kwamba hakuna uchaguzi mwingine. Alisema kwa upande wao wapo katika maandalizi ya uchaguzi mwingine ikiwemo kutayarisha mawakala watakaosimamia uchaguzi huo.
Hivi karibuni wakati akilihutubia Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano huko Dodoma, Rais John Magufuli alisema kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa vyama vya siasa hususan CCM na CUF atahakikisha majaribu ya kisiasa yaliyopo yanamalizwa kwa njia ya amani na utulivu.
Tayari mazungumzo yenye lengo la kuepusha mpasuko wa kisiasa baada ya kfuutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 yamekuwa yakiendelea hapa kwa nyakati tofauti yakiwahusisha wagombea urais, Dk Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF. Shein ndiye Rais wa Zanzibar kwa sasa wakati Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais