MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imetupa pingamizi lililowekwa na Serikali katika shauri la kuzuia kuagwa kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa hivi karibuni na watu wasiojulikana.
Kesi hiyo ya madai namba 10 ya mwaka huu ya kuiomba Mahakama Kuu itoe ruhusa ili ombi la mlalamikaji lisikilizwe, ilisikilizwa jana na Jaji Lameck Mshana, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza na kwa upande wa serikali iliwakilishwa na Mawakili wa Serikali wakuu Sethi Mkemwa na Emily Kiria na kwa upande wa utetezi iliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na John Mallya.

Awali, akiwasilisha hoja ya kuiomba mahakama kutengua pingamizi lililowekwa na mjibu maombi wa kwanza, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza na mjibu maombi wa pili Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa utetezi, Mallya alisema hoja yao haina sababu za msingi za kumzuia mlalamikaji, Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa Mawazo kumzika marehemu kwa kuwa alikuwa ndiye mlezi wake.
Naye Kiria aliiomba mahakama kutokukubali hoja hiyo kwa madai kuwa wamepitia kiapo kilichowasilishwa na mlalamikaji na kugundua kuwa yeye ni baba mdogo wa marehemu na hakuna sehemu inayoonesha wazazi wake Mawazo walifariki dunia na kwamba inaonyesha Mawazo alizaliwa Sengerema katika Kijiji cha Butundwe (ambapo kwa sasa ni Mkoa wa Geita) na kuthibitisha hilo marehemu asingezikwa Geita, bali jijini Mwanza.
Hata hivyo, Jaji Mshana aliitupilia mbali hoja na kuuomba upande wa mlalamikaji kuwasilisha hoja ya msingi ya kupeleka maombi ya msingi ya kufunguliwa kwa kesi hiyo. Alisema kutokana na umuhimu wa hoja inayogusa maisha ya watu, mahakama iliona ni vyema hoja hiyo katika hatua za awali isikilizwe zote mbili.
Alisema kwa vile mlalamikaji katika kesi hiyo ni baba mdogo wa marehemu na kwa mujibu wa mila na desturi za kiafrika baba mdogo ni mtu anayehusiana moja kwa moja na msiba wa mtoto wake na hawezi kujifanya mgeni katika suala hilo.