CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza utendaji wa Rais John Magufuli tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, kwa kuishi kwa kauli na ahadi zake.
Mwenyekiti wa CCM anayemaliza muda wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema hayo jana alipohutubia maelfu ya wanachama wa chama hicho na wananchi wa Mkoa wa Singida kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM.
Akizungumza katika Uwanja wa Namfua, Kikwete alisema Rais Magufuli anastahili hongera kwani Watanzania wanafurahi kuona akiishi kwa kauli alizotoa wakati wa kampeni na wakati akizindua Bunge.

“Hongera Rais kwa kazi nzuri uliyoanza nayo, watakaopinga utekelezaji wa ahadi zako unaoendelea, wanaipinga CCM...kuna mtu aliniuliza mbona huyu (Rais Magufuli) anafanya hivi, nikamjibu kasome Ilani,” alisema Kikwete.
Alisema hatua zote zilizochukuliwa na Rais Magufuli, zina baraka zote za chama na ndiyo mambo ya msingi yaliyoelezwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. “Mimi binafsi, viongozi wa chama na chama, tunakuunga mkono katika mambo unayotekeleza, CCM ndiyo inachotaka ufanye na kimo ndani ya Ilani yetu ya mwaka 2015,” alisema Kikwete.
Kikwete alisema katika siku 90 za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Magufuli, amedhihirisha kuwa yeye ni mtekelezaji makini wa Ilani ya chama hicho na kazi aliyoanza kuifanya, ndiyo aliyotakiwa kuifanya kwa nafasi yake ya mshika bendera wa CCM.
Akitoa mifano, Kikwete alisema Ilani ya CCM imetaka Serikali yake iendeleze vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma na kuchukua hatua za haraka kwa wahusika, kazi ambayo Rais Magufuli ameifanya.
Kwa mujibu wa Kikwete, Ilani hiyo pia imeitaka Serikali yake iimarishe vyombo na taasisi za kupambana na rushwa na kuanzisha Mahakama Maalumu ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hatua ambayo aliisemea na mara ya mwisho aliizungumzia juzi katika Siku ya Sheria, alipomueleza Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, achukue hatua.
Kikwete alisema utendaji mzuri wa Rais Magufuli umesababisha vyama vya upinzani, alivyoviita watani wa CCM, kukosa cha kusema na kuishia kudai kuwa Serikali inatekeleza Ilani yao.
Mwenyekiti huyo wa CCM alihoji, kama Rais Magufuli anatekeleza Ilani ya vyama hivyo vya upinzani, kwa nini viongozi wake wakiwemo wabunge wao hawamuungi mkono, maana alipokwenda kuzindua Bunge, walitoka nje na kujionesha walivyo watu wa hovyo.
Pamoja na utekelezaji mzuri wa Serikali, Kikwete alihadharisha kuwa wana CCM wanapaswa kuendelea kutoa maoni kuhusu utekelezaji huo, hasa ikitokea utekelezaji unafanyika ndivyo sivyo na kusababisha watendaji wa Serikali na chama waonekane wabaya.
Alifafanua kwamba jambo linalotekelezwa linaweza kuwa jema kabisa, lakini utekelezaji ukiwa mbaya, linaweza kuonekana ni kero, hivyo wanachama wana haki ya kulizungumzia na hasa kama kuna watendaji wanaofanya makusudi ili chama kionekane kibaya.
JK aaga
Rais mstaafu huyo pia alitumia nafasi hiyo kuaga rasmi wanachama wote wa CCM, aliposema kwamba hiyo itakuwa mara yake ya mwisho kuhutubia kwenye maadhimisho hayo katika nafasi ya Mwenyekiti wa chama, kwa kuwa maadhimisho kama hayo mwakani, yatahutubiwa na Rais Magufuli, ambaye atakabidhiwa kijiti cha Mwenyekiti wa chama.
“Pia nitumie fursa hii kuwaaga rasmi katika nafasi hii ya Mwenyekiti wa CCM, namwachia kijiti Rais Magufuli na mwakani kwenye maadhimisho kama haya, ndiye atakuwa Mwenyekiti wa chama, mimi nastaafu uongozi,” alisema Kikwete.
Alisema anafurahi kuondoka madarakani akikiacha chama kiko imara na kitaendelea kuwa imara, kwani ndicho chama chenye sura ya kitaifa na sura ya dhati ya Muungano, hivyo wananchi hawana shaka nacho na wale wote waliodhani chama kitamfia, wafahamu kwamba chama ndio kinazidi kuimarika na kujiunda upya.
Hatua maumivu
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrhaman Kinana, alisema wananchi wanapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa hatua anazochukua za kukataa mbinu za kitapeli za kurudisha kasi ya kijitegemea nyuma.
“Rais Magufuli anasukumwa na uzalendo alionao kwenye maamuzi yake na baadhi ya hatua anazochukua zina maumivu, lakini tiba lazima ipatikane na ni jukumu letu sote kumuunga mkono, peke yake hataweza,” alisema Kinana.
Upinzani kusahaulika
Akizungumza kabla ya hotuba ya Mwenyekiti, Rais Magufuli alisema Serikali anayoiongoza itatekeleza Ilani ya CCM na kuondoa kero zote za wananchi, ili hata wale wanaofikiria vyama vingine na wale wanaoota vyama hivyo wasifikirie wala kuota vyama hivyo.
Alisema ni lazima watendaji wote ndani ya Serikali, watekeleze Ilani ya CCM na kuondoa kero za wananchi, kwani CCM ndiyo iliyomuweka madarakani na kwa asiyetaka kutii hilo akae pembeni.
Alitoa mfano CCM Mkoa wa Singida kujitolea madawati 1,000 ili kuondoa kero ya wanafunzi kukaa chini, akasema chama kimeonesha njia na kuagiza wakuu wa mikoa na wilaya, wapunguze safari zisizo na tija, ili fedha hizo zikanunue madawati, ili wanafunzi wasikae chini.
“Kuanzia sasa kama shule itaendelea kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na wakurugenzi wa eneo husika, hali hiyo itakuwa kipimo kwamba hawajui kazi, kwa sababu haileti maana ofisi zetu ziwe na viyoyozi na viti vya kuzunguka, wakati jirani kuna shule watoto wanakaa chini,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.
Alisema hilo atalisimamia kwani Ilani ya CCM, inazungumzia suala la elimu na mambo mengine muhimu ambayo Serikali imeanza kuyafanyia kazi na kusema hayuko tayari kuona mtu au watu wanaikwamisha.