RAIS John Magufuli amecharuka na kuitaka Idara ya Mahakama kushughulikia kwa kasi kesi zinazohusu uhujumu uchumi na ufisadi ili jitihada za Serikali za kupambana na matatizo hayo, zizae matunda.
Pia amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa sasa kipaumbele chake ni kutenga na kupeleka fedha katika maeneo yenye uhitaji kwa maslahi ya wananchi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Pamoja na hayo, ametetea maamuzi yake ya kuwasimamisha baadhi ya watendaji wanaotuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya na kusisitiza kuwa amelazimika kuchukua hatua hizo kwa maslahi ya Watanzania na si udikteta, kama baadhi ya watu wanavyodai.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria nchini Dar es Salaam jana, Dk Magufuli alisema ili Serikali ifanikishe azma yake ya kupambana na mafisadi na wahujumu uchumi, ni lazima Idara ya Mahakama iweke uzalendo mbele na kujipanga kushughulikia kesi hizo kwa dhati.
Alisema Sheria na Mahakama, ndio njia pekee ya kutoa haki, hivyo kama moja ya mihimili mikuu nchini ni vyema idara hiyo ikatumia haki katika kusikiliza kesi hizo kwa haraka kwa kuwa watuhumiwa wake wengi ndio waliofikisha nchi mahali pabaya.
“Najua watuhumiwa wa kesi hizi wengi wao wana fedha nyingi lakini ninaamini kuwa mtawatendea haki Watanzania, naomba mahakimu na majaji mtangulize Tanzania kwanza na uzalendo ili haki itendeke na kuwaokoa Watanzania wengi,” alisisitiza Dk Magufuli.
Mlundikano wa kesi Alisema kwa taarifa alizonazo hadi jana kuna kesi takribani 442 zinazohusu watu waliokwepa kulipa kodi, ambazo endapo zitaamuliwa gharama yake itakuwa ni takribani Sh trilioni moja.
Alisema kesi hizo za tangu mwaka 2011 hadi leo hazijaamuliwa, hali inayosababisha kuwepo na wakwepa kodi wengi kwani wanapobanwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hukimbilia mahakamani, ambako kesi zinachukua muda kupatiwa ufumbuzi.
Dk Magufuli alisema endapo kesi hizo zitaamuliwa hivi karibuni, Serikali itaingiza kiasi hicho cha Sh trilioni moja na hivyo kuwezesha kupatikana kwa ufumbuzi wa ndege za Serikali, kwani zinaweza kununua ndege aina ya Airbus takribani saba ambapo ndege moja inauzwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 90.1.
“Lakini pia fedha hizi zinaweza kuondoa changamoto ya uhaba wa fedha inayoikabili idara hii ikiwemo kupatikana kwa fedha za kuendeshea kesi mbalimbali zilizokwama kutokana na ukosefu wa fedha na kuboresha idara hiyo hasa katika maeneo ambayo mahakama zimechakaa,” alifafanua Rais.
Pamoja na kesi hizo, Rais pia alibainisha kuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Dar es Salaam, kuna kesi takribani 26 ambazo wahusika wake walishikwa na uthibitisho wa kukutwa na nyara za Serikali.
Alibainisha kuwa pamoja na kukutwa na uthibitisho wa nyara hizo, kesi hizo zimechukua takribani miaka mitano sasa bila kutolewa uamuzi wowote huku upande wa mashtaka (Mkurugenzi wa Mashtaka nchini - DPP) na Polisi, wakidai kuwa uchunguzi unaendelea.
“Hali hii inasikitisha, hivi mtu unachunguza nini wakati mtu ameshikwa na kila kitu kina uthibitisho? Wapelelezi wapo na DPP yupo, natumaini katika hili tatizo limeonekana liko wapi. Mtu akishikwa red handed (na uthibitisho) afungwe mnahitaji upelelezi gani au ndio mbinu zenyewe za kuombea rushwa? alihoji.
Alisema ili Serikali ifanikiwe katika vita dhidi ya wahujumu uchumi na mafisadi, lazima vyombo vyote vya dola vinavyohusika kwa maana ya Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na DPP vitimize wajibu wao kwa uaminifu.
Alimtaka Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman ahakikishe ndani ya siku chache kuanzia jana, kesi 442 za uhujumu uchumi na ufisadi zinasikilizwa na kutolewa hukumu na endapo atafanikisha agizo hilo, atapatiwa na Serikali robo ya Sh trilioni moja zitakazopatikana kutokana na kesi hizo, ambayo ni Sh bilioni 250 na fedha inayobaki Sh bilioni 750 ataipeleka kununulia ndege za Serikali.
Aidha, alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, kuiagiza Wizara ya Fedha ndani ya siku mbili zijazo, iwe imeipatia Idara hiyo ya Mahakama kiasi cha Sh bilioni 12.5 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya idara hiyo ili ifanikishe na kutekeleza majukumu yake.
“Haiwezekani nchi yetu iwe masikini wakati tuna utajiri wa rasilimali. Leo hii watalii wanashukia Kenya na kuishia huko kwa sababu eti hatuna ndege yetu wakati uwezo wa kuwa nayo tunao. Inashangaza Tanzania ndio wazalishaji wa tanzanite lakini wanaoongoza kuizalisha duniani ni India na Kenya. Jamani hii ndio Tanzania yetu, naagiza haya kwa sababu nataka mabadiliko,” alisisitiza.
Alisema inamuuma kuona Watanzania tunaomba misaada wakati uwezo wa kujiendesha wenyewe kama nchi upo.
“Inaniuma sana hivi jamani Watanzania tuna ugonjwa gani? Ndio maana nasisitiza tunahitaji tuombewe na atakayetukwamisha wakati tunasonga mbele ashindwe na alegee,” alieleza Dk Magufuli.
Alisema hata ndani ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, alibaini kuwepo kwa kesi 556 ambazo hazijatolewa hukumu, eti kwa sababu Msajili ameshindwa kuandika barua na kupeleka mafaili ya kesi Mahakama Kuu ili zitolewe uamuzi.
“Haya yanafanyika Kamishna wa Ardhi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Msajili wapo. Hii ndio Tanzania bwana,” alieleza katika njia ya masikitiko.
Akaunti za mabenki, BoT
Aidha, Rais alisema pia Serikali yake imebaini kupitia benki takribani 54 zilizopo nchini, watendaji wakuu wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu wanaokaa na fedha, hufungua akaunti katika benki hizo, na baadaye benki hizo hutumia fedha hizo kuombea mikopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alisema hali hiyo ni sawa na Serikali kufanya biashara na fedha zake yenyewe, huku akitaja baadhi ya taasisi zinazoweka kiasi kikubwa katika benki hizo kuwa ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Aliagiza taasisi zote za Serikali, zifunguliwe akaunti BoT ili fedha za Watanzania zitumike kulingana na mahitaji ya wananchi wake.
“Wapo watendaji waliitumia vibaya fursa hii, walikopeshana na walilipana riba sasa hivi hakuna tena haya, ndio maana baadhi ya watu kwa wingi wa fedha walizokuwa nazo walikuwa wakiipelekesha Serikali,” alisema.
Mahakama ya mafisadi
Aliitaka idara hiyo kuharakisha mchakato wa kuanzisha Mahakama itakayoshughulikia wahujumu uchumi na mafisadi (Mahakama ya Mafisadi), kwani kadri muda unavyokwenda na mahakama hiyo inavyochelewa, ndio mafisadi hao wanavyozidi kuichezea nchi.
“Mimi si kichaa na si dikteta, ila nalazimika kuchukua hatua kutokana na hali halisi, haiwezekani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itumie shilingi bilioni 70 na kutengeneza vitambulisho milioni 22.7 halafu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa itumie shilingi bilioni 177 na kutengeneza vitambulisho milioni mbili, hii kweli inaingia akilini?” Alihoji.
Aliipongeza idara hiyo ya Mahakama kwa kuweka kipaumbele katika kubana matumizi na kuachana na masuala yasiyo ya lazima, ikiwemo kutoirusha moja kwa moja kwenye televisheni sherehe hiyo ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria.
“Kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni ni shilingi bilioni nne, wakati nyie kwa sasa mnahitaji shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuendesha kesi za uchaguzi. Kupanga ni kuchagua, kwa kiongozi makini lazima afikirie wapi apeleke fedha kwanza na wapi pa kupanyima, huo ndio uongozi,” alisisitiza.
Mahakimu 508
Aidha, alimtaka Jaji Mkuu kutowabembeleza mahakimu takribani 508 wanaodaiwa kutotimiza viwango, vilivyowekwa vya usikilizaji kesi na badala yake awachukulie hatua stahiki kwani Tanzania ina wasomi wengi wenye sifa ya Sheria wanaosubiri ajira wakati wowote.
Mahakimu hao walishindwa kutimiza vigezo vya kusikiliza takribani kesi 260 kwa mwaka, kama Jaji huyo alivyowapangia na hivyo kupewa siku saba wajieleze kwanini hawakufanikisha malengo hayo.
“Siingilii Mahakama lakini kwa mtazamo wangu hawakupaswa kukiuka maagizo yako Jaji Mkuu tena uliyeniapisha mimi,” alieleza.
Kauli ya Jaji Mkuu
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Othman alisema idara hiyo imejipanga kwenda na kasi ya Rais Magufuli kupitia kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na katika kuhakikisha inapunguza mlundikano wa kesi, ameagiza kuanzia Januari mwaka huu mahakama zote za mwanzo na wilaya, kesi zao zisidumu zaidi ya miezi sita.
Kesi za ubunge, udiwani
Jaji Mkuu alisema tayari Mahakama imejipanga kumaliza kesi zote za uchaguzi hadi Juni mwaka huu, na tayari imepanga kusikiliza kesi 20 za wabunge.
Tangu uchaguzi huo umalizike Oktoba mwaka jana jumla ya kesi 221 zilifunguliwa kati ya hizo 53 ni za ubunge na 173 madiwani na jumla ya Sh bilioni tatu zinahitajika kukamilisha usikilizaji wake.
Alisema kwa sasa Idara ya Mahakama inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kwani kuanzia mwaka wa fedha wa 2014 na 2015 walipatiwa fedha takribani Sh bilioni 40, lakini mwaka wa fedha unaoishia mwaka huu fedha hizo zilipunguzwa na kufikia Sh bilioni 12.5 ambazo hadi jana zilikuwa hazijatolewa.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura aliomba ushirikiano wa Serikali katika kusimamia na kuhakikisha kesi zinazohusu uimarishaji wa fani hiyo, zinaamuliwa mapema ili kukuza tasnia hiyo.