Utawala nchini Somalia umetoa Video inayoonesha watu wawili wakimkabidhi abiria mmoja anayeshukiwa kuwa mlipuaji wa kujitolea mhanga kitu kinachoonekana kama Laptop kabla ya mlipuaji kuabiri ndege hiyo iliyokumbwa na mkosi huo.
Msemaji wa serikali anasema kuwa watu hao ndio washukiwa wakuu katika ulipuaji uliotokea juma lililopita kwa ndege ya abiria ilipolazimika kutua kwa dharura baada ya bomu kulipuka ikiwa angani.

Inasadikika kuwa mmoja kati ya watu walioleta kipakatilishi hicho alikuwa ni mfanyikazi wa shirika linalohudumu katika uwanja huo wa ndege wa Mogadishu.
Image copyrightHarun Maruf
Image captionVideo inayoonesha watu wawili wakimkabidhi abiria mmoja anayeshukiwa kuwa mlipuaji wa kujitolea mhanga kitu kinachoonekana kama Laptop
Bwana Abdisalam Aato anasema kuwa kifaa hicho kinachofanana na Kipakatilishi ndicho kinachoshukiwa kuwa ni kilipuzi kilichosababisha ndege ya Daallo Airlines kurejea ardhini mara moja muda mchache baada ya kupaa ikiwa na abiria.
Takriban watu 20 wamekamatwa wakiwemo wale wawili walionaswa kwenye video hiyo .
Image copyrightHarun Maruf
Image captionMsemaji wa serikali anasema kuwa watu hao ndio washukiwa wakuu katika ulipuaji uliotokea juma lililopita
" Kwa uchache watu 20 , wakiwa pamoja na wale wawili walionekana katika kanda hiyo ya video walikamatwa kwa kuhusika o na mlipuko katika ndege hiyo , '' Aato aliiambia AP.
Mlipuko huo ulisababisha shimo kubwa katika ubavu wa ndege hiyo karibu na hifadhi ya mafuta upande wa kulia uliomlazimu rubani wa ndege hiyo aina ya Airbus 321 iliyokuwa ikielekea Djibouti kuirejesha katika uwanja wa ndege wa Mogadishu Somalia.
Hakuna aliyeuawa katika tukio hilo ijapokuwa kumekuwa na habari ambazo hazikuthibitishwa kuwa mtu mmoja alitupwa nje ndege hiyo ilipokuwa angani