Kamishina wa Nec, Asina Omary
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema uelewa mdogo kuhusu upigaji kura na umuhimu wake katika majimbo manane, kati ya hayo manne ya Dar es Salaam, umesababisha idadi ya wapigakura kuwa ndogo kuliko ilivyotarajiwa.
Miongoni mwa majimbo hayo ni Ubungo, Kawe, Mbagala, Temeke, Kilindi, Handeni, Kavuu, Nzega Vijijini ambako wapigakura waliojitokeza kupiga kura walikuwa kati ya asilimia 34 hadi 49.
Kamishina wa Nec, Asina Omary, amesema hayo juzi mjini hapa wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa tathmini kati ya Tume na asasi za kiraia zilizopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia zilizopewa kibali cha kutoa elimu hiyo kutoka mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Pemba , Unguja na Morogoro walishiriki mkutano huo.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, baadhi ya vijana waliokuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa waliendesha kampeni za chini kwa chini kuhakikisha wazee na wanawake ambao walionekana kutokuwa upande wao hawapigi kura kwa kuwanyang’anya ama kuwaibia kadi za kupiga kura.
Hivyo alitolea mfano wa maeneo ambayo ziliendeshwa kampeni za chini kwa chini kwa malengo hayo ni Tarime, Rorya, Loliondo, Ngorongoro, Hanang na Simanjiro.
“ Uharibuji wa kura, baadhi ya wapiga kura walikuwa wanaweka alama ya V kwa mgombea anayemtaka na kuweka X kwa mgombea asiyemtaka na hivyo kupelekea kura nyingi kuharibika,” alisema Kamishina huyo katika uwasilishaji wa mada yake.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, maeneo ambayo yameharibu kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu huo ni Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kura 28,961 na majimbo mengine kura zake katika mabano ni Misungwi (14,941), Dodoma Mjini (9,992), Ubungo ( 8,678), Kinondoni ( 6,782) na Ukonga kura 6,620.
Alisema, licha ya mafanikio ya ushirikiano wa Tume na Asasi za Kiraia, Tume inatoa rai kwa Asasi za Kiraia nchini kuweka maslahi ya taifa mbele kwa kufuata sheria ili kuleta mshikamano na kudumisha amani na utulivu vilivyojengeka kwa miaka mingi.
Hivyo alisema, Tume inatarajia kuwa Asasi za Kiraia zitaendelea kutoaushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendeleza utoaji wa elimu kwa Watanzania na hatimaye kukuza Demokrasia nchini.
Pamoja na hayo alizitaka , Asasi za Kiraia pia kushiriki kikamilifu Kuwaelimisha wananchi juu ya haki na wajibu wao katika michakato mbalimbali ya chaguzi ikiwemo uandikishaji wa wapigakura, uchaguzi wenyewe na hata katika kura za maoni.