Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi
{pichani}
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa taarifa ya maendeleo ya msako unaofanywa dhidi ya majangili, waliomuua rubani wa ndege iliyokuwa ikifanya doria katika Pori la Akiba mkoani Simiyu na kusema umefikia hatua muhimu na hivi karibuni wahusika watakamatwa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gaudence Milanzi alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari mjini hapa, akisisitiza kwamba Serikali itashinda vita dhidi ya ujangiri hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
Pamoja na taarifa hiyo, Katibu Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya maswali mbalimbali yaliyojitokeza baada ya tukio hilo, ikiwemo madai kwamba kulikuwa na mizoga mingi ya tembo katika hifadhi hiyo na walichelewa kutoa msaada.

“Msako umefikia hatua muhimu na kasi iliyooneshwa, hivi karibuni wahusika wote watakamatwa,” alisema na kupongeza watumishi wanaohusika na msako kwamba wamefanya kazi usiku na mchana bila kujali mazingira magumu, ikiwemo mvua.
Akisisitiza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kwamba msako ufanyike na wahusika wakamatwe mapema iwezekanavyo, alisema kazi hiyo imefanywa na wizara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Alisema yeye pia aliagizwa na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe afanye ziara kufuatilia maendeleo ya msako, jambo ambalo alitekeleza na kuikamilisha juzi.
Aliendelea kusema, “ziara nimeikamilisha juzi jioni...nimefarijika msako wa wahalifu unaendelea vizuri kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani na vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa (Simiyu) na kitaifa.”
Akizungumzia muda ambao msaada ulipatikana baada ya ndege kuanguka, alisema juhudi zilichukuliwa kuhakikisha msaada unapatikana kwa kutumia doria nyingine kwenye eneo la tukio ndani ya saa mbili.
Alisema kutokana na eneo hilo la Pori la Akiba la Maswa na Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba kuwa na mito, wengine waliokwenda kutoa msaada iliwabidi waogelee.
Upande wa madaktari ambao alisema walitoka Arusha na wengine Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu alisema walifika baada ya saa tano.
Kuhusu hatma ya mabaki ya ndege katika eneo hilo, mtendaji huyo wa Wizara alisema yatachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika. Alisema yamefunikwa na yako chini ya ulinzi, kuepusha ushahidi kuingiliwa.
Akifafanua idadi ya mizoga ambayo ndege hiyo ilishuhudia kabla ya kuanguka, alisema ulikuwa moja tofauti na madai kwamba ilikuwapo mizoga mingi. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, rubani aliyepoteza maisha, aliajiriwa na Kampuni ya Mwiba Holdings ambao wamemilikishwa kitalu cha kupiga picha za utalii.
Alisema kampuni hiyo, pia ina jukumu la kufanya ulinzi na kuhifadhi. “Hilo ni jukumu la kawaida kwa kampuni zinazomilikishwa vitalu...mara nyingi huwa wanafanya joint patrols (doria ya pamoja) pamoja na askari wetu,” alifafanua.
Alisema mwili wa rubani huyo ulitarajiwa kusafirishwa jana usiku kwenda kwao Uingereza. Serikali imetoa pole kupitia ubalozi wa nchi hiyo.