Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imehakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika kwa amani na kuwahimiza wajitokeze kwa wingi kushiriki siku itakapofika.
Naibu Waziri, Hamad Yussuf Masauni alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM).
Mbunge Tahir katika swali la nyongeza, alisema kwa kuwa Zanzibar inajiandaa na Uchaguzi Mkuu, ni vyema serikali ikazipatia wilaya za Magharibi A na B magari ya kwa ajili ya vituo mbalimbali vya Polisi.

Tahir ambaye alisisitiza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar si jambo geni kwa kuwa hata mwaka 1961 ulifutwa ukarudiwa mwaka 1963, alisisitiza kwamba kuvipatia vituo hivyo magari, itapunguza watu alioita ‘mazombi’.
Naibu Waziri aliwahakikishia Wazanzibari kwamba Serikali itaimarisha usalama kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kuhimiza wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
“Hapatakuwa na uvunjifu wa amani,” alisema.
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Dimani, Tahir, Naibu Waziri Masauni alikubaliana na mbunge huyo kwamba wilaya hizo za Magharibi A na B hazina magari na mafuta ya kutosha kwa shughuli za Polisi.
Alisema hali hiyo ni changamoto kwa vituo vingi vya polisi nchini, lakini akaongeza kuwa mgawo wa vitendea kazi ikiwemo magari huzingatia jiografia ya wilaya, hali ya uhalifu na idadi ya watu wanaohudumiwa na kituo husika na si idadi ya vituo vidogo vilivyopo katika wilaya husika.
Masauni alisema, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakusudia kuwasilisha bajeti mbele ya Bunge kuboresha hali ya vyombo vya usafiri, mafuta na vilainishi kukidhi mahitaji halisi ya Polisi nchini.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema ufumbuzi wa suala la Zanzibar haupo kwenye Bunge, wala ofisi za mabalozi wa kigeni, bali upo ndani ya katiba na sheria za Zanzibar.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema hayo juzi bungeni mjini hapa, wakati akichangia mpango wa maendeleo wa Taifa.
Alisema ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Zanzibar, haliwezi kumalizwa ndani ya Bunge, kwenye ofisi za kibalozi wala barabarani bali upo ndani ya Katiba. Pia alisema Muungano utaendelea kudumu na amani ya nchi itadumu na kwamba nchi itaendelea kuwa ya amani na wananchi wataendelea kufanya shughuli zao bila ya kubugudhiwa.
January alisema Rais John Magufuli anafanya kazi kubwa, hali iliyosababisha aungwe mkono kila sehemu, hivyo si dhambi na wapinzani wakimuunga mkono.
Wakati January akisema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema suala la Zanzibar ni vyeti na Katiba inatambua serikali mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar. Alisema Katiba ya Zanzibar, si ya Muungano lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahusika hadi Zanzibar.
Masaju alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haipaswi kuingilia masuala ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, isipokuwa kwa mambo ya Muungano tu. Pia aliwataka baadhi ya wabunge kuacha tabia ya kuhamasisha wananchi kufanya vurugu. Imeandikwa na Stella Nyemenohi na Sifa Lubasi, Dodoma