Polisi nchini Kenya inaendelea na msako wa kuutia mbaroni mtandao wa kundi la wapiganaji la ISIS ambalo linataka kukita mizizi yake nchini Kenya kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wananchi wasio kuwa na hatia. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na inspekta mkuu wa polisi .

Kauli hiyo imetolewa baada ya polisi nchini Kenya kuwatia mbaroni watu wawili wanaoshukiwa kuwa ni wafuasi wa kundi la wapiganaji la ISIS.
Kwa mujibu wa polisi, kukamatwa kwa wawili hao ambao ni Mwangolo Mgutu na Abubakar Jillo Mohammed kumezuia mashambulizi ya kigaidi yaliyokuwa yakipangwa kwa kutumia vilipuzi na silaha nyingine katika mji wa Nairobi na Mombasa.
Mbali na kukamatwa kwa washukiwa hao wawili, polisi pia imepata vitu mbalimbali katika nyumba ya Kiguzo Mwangolo kama vile misumari, betri, waya na mbolea ambazo inadaiwa zingetumika kutungezea bomu la nyumbani.
Polisi imeendelea kusema, katika uchunguzi wake wa mwanzo, imebaini kuwa Kiguzo na Abubakar ni miongoni mwa waandishi wa makala iliyokuwa inasambaa kupitia mtandao ambao ilikuwa ikielezea kuwepo kwa kundi la Jahba katika eneo la Afrika Mashariki ambalo limetangaza kumuunga mkono kiongozi wa ISIS Abubakr Al-Baghdadi.