Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
MBUNGE wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM) amesema Bunge linapaswa kufahamu ni mbunge gani ambaye anajihusisha na ujangili, kwani hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria.
Magige, ambaye amependekeza sheria ibadilishwe majangili ama wapigwe risasi au wafungwe jela maisha, ni miongoni mwa wabunge ambao walivalia njuga suala la ujangili jana wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kwa upande wake, serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema majangili nguli wanane wenye mitandao ya kimataifa ni miongoni mwa wahalifu 53 waliohukumiwa baada ya kukutwa na hatia.
Wabunge majangili? Akichangia, mbunge Magige alisema inasemekana baadhi ya wabunge wanajihusisha na ujangili hivyo akashauri ni vyema wakafahamika. “Inasemekana baadhi ya wabunge wanajihusisha na ujangili. Huyo jangili ni nani? Munde Tambwe, Catherine Magige au Ally Keissy,” alihoji mbunge huyo wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Arusha. “Hakuna aliye juu ya sheria, tunaambiwa majangili tunao humu ndani, tunataka tuwafahamu, tusinyooshee vidole wengine,” aliongeza Magige.
Alisema ujangili umekithiri nchini na tembo wanatoweka. Alipendekeza sheria ibadilishwe majangili ama wapigwe risasi au wafungwe jela maisha. Majangili nguli watajwa Profesa Maghembe alisema katika mwaka 2015/16, doria zilifanyika ndani na nje ya Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu kwa siku-doria 109,474 na ziliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 1,176 na kesi 654 zilifunguliwa.
“Kesi 161 zilimalizika kwa wahalifu 53 kuhukumiwa kifungo cha jumla ya miezi 6360 na shilingi 363,904,800 kulipwa kama faini. Kati ya wahalifu waliohukumiwa, wanane ni majangili nguli wenye mtandao wa kimataifa,” alisema waziri. Alisema katika doria zilizofanyika, nyara mbalimbali za serikali zilikamatwa, ambazo ni pamoja na wanyamapori hai; mijusi 315, kobe 202, tumbili 81 na nyani mmoja.
Nyara nyingine ni vipande 253 vya meno ghafi ya tembo vyenye uzito wa kilo 634 na vipande 34 vya meno ya tembo yaliyochakatwa vyenye uzito wa kilo mbili. “Vilevile, kilo 10,096 za nyamapori wa aina mbalimbali na ngozi 39 za wanyamapori zilikamatwa.
Aidha, bunduki 85 na risasi 1,235 za aina tofauti zilikamatwa,” alisema Maghembe. Katika kudhibiti ujangili wa wanyamapori, wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi ilibaini kuwa ujangili unafanyika katika ngazi tano.
Alitaja ngazi hizo kuwa ni baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi na watumishi wasio waaminifu. “Wawindaji haramu wanaojihusisha moja kwa moja na kuua wanyama, wasafirishaji na madalali, wawezeshaji kwenye ngazi ya nchi wanaonunua nyara, kusambaza vitendea kazi (silaha) ambao ni kiungo kati ya majangili nguli na watakatishaji fedha na wahalifu walioainishwa katika ngazi tatu za awali na majangili nguli wa kimataifa,” alisema.
Alishukuru mamlaka zinazosaidiana nazo katika vita dhidi ya ujangili ambavyo ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Kikosi cha Kuzuia Makosa Makubwa na mhimili wa Mahakama. Wahoji aliyetoa leseni Wakati huo huo, katika uchangiaji, wabunge wamekuja juu na kuibana serikali wakitaka kufahamu ni nani aliyeipa tena leseni Kampuni ya Green Miles Safaris Limited baada ya kufutiwa kwa kujihusisha na uwindaji haramu.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) alihoji ni nani aliyeipa tena leseni Kampuni ya Green Miles Safaris Limited kwa sababu leseni yao ilishafutwa. “Hili la Green Miles Safaris Limited nalijua…ilikiuka taratibu za uwindaji wa wanyamapori na ilikuwa disqualified.
“Ilinyang’anywa leseni, nilikuwa kwenye Tume…wataalamu wa wizara watoe maelezo,” alisema mbunge huyo wa Kasulu. Katika maoni yao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge pia ilihoji suala hilo ikisema kampuni hiyo ya uwindaji ilinyang’anywa leseni kutokana na uwindaji usiozingatia sheria na taratibu.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inashangaa ni kwa nini mheshimiwa waziri wa sasa kwa barua yake ya Mei 9, 2016 inaonekana kuwa inaipatia tena kampuni hiyo kitalu cha uwindaji wakati tayari ilikwisha pokonywa leseni kwa kuwa ilivunja sheria,” alisema Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Esther Matiko.
Katika mchango wake mwingine, Nsanzugwanko alipendekeza serikali kuwaondoa kwa ustaarabu mifugo inayoingia katika maeneo ya hifadhi. Aidha, alishauri kuwa serikali iyagawe maeneo yasiyo na tija ya hifadhi ambayo yako kwa muda mrefu na hayatumiki kwa kuyahuisha na kuwapa wananchi ili wafanye shughuli za maendeleo.
Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (CCM), alikataa kuunga mkono hoja hiyo akisema wananchi wake wanauawa na mifugo inauawa katika mapori ya akiba ya Muyowosi na Kigosi. Biteko alisema ng’ombe 125 na punda wameuawa na ng’ombe 603 wametaifishwa na kuna unyanyasaji mkubwa wa wananchi wanaooingia katika hifadhi. Alisema ziko nyumba 40 ziko katika vijiji ambavyo vimeandikishwa kisheria, hivyo wana haki zote kisheria, lakini wananyanyaswa na askari wa wanyamapori.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) pia alalamikia unyanyasaji wa askari wa wanyamapori akisema kuna vijiji 21 vimeandikishwa katika jimbo lake, lakini watu wake wanaoishi kwa hofu kubwa. Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema Bunge linapaswa kujisafisha kuhusu tuhuma za kuwa kuna mbunge ni jangili.
Msigwa alisema tuhuma hizo ni kashfa kwa Bunge kwa sababu suala hilo limekuja huku chombo hicho cha kutunga sheria kikiwa kimewahi kutuhumiwa kuwa kuna wala rushwa na walevi. “Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hapa mbunge mmoja amesema asubuhi kuwa kuna mbunge ni jangili. Magazeti yameonesha kuwa gari zake zimetumika katika ujangili.
Bunge lazima lisafishwe katika hili, maana Bunge hili limewahi kutuhumiwa kwa rushwa na kuwa wengine ni wanapiga mtindi,” alisema Msigwa. Alisema ni lazima Bunge lijisafishe kwa tuhuma hizo, kwani pia mbunge anayetuhumiwa kwa kuwa jangili, anatajwa kuvamia eneo la hifadhi yawanyamapori wilayani Meatu. Alisema si sahihi kwa mtu kuchimba madini ndani ya hifadhi,hivyo anataka kufahamu mbunge huyo amepewaje eneo la kuchimba madini humo.
Aidha, Msigwa alizungumzia suala la Kampuni ya Green MilesSafaris Limited, akihoji kuwa kampuni hiyo ilipokonywa leseni za uwindaji kwa kukiuka taratibu, nani amewapa tena leseni hiyo. “Kampuni hii haina sifa kwa sababu imekiuka uhifadhi,haikupewa vitalu, haina sifa, imefanya infringement zaidi ya 11, hawana sifa za uwindaji.
Tujue nani Operesheni Tokomeza Alitaka ripoti ya Tume Maalumu ya Kimahakama iliyoundwa kufanya tathmini ya Operesheni Tokomeza kuwekwa hadharani na kumtaka Spika aombe kwa serikali ili iwekwe hadharani.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Kambi ya Upinzani ikisema ni wakati mwafaka sasa kuelewa ni majangili wangapi kuelezwa baada ya operesheni hiyo kumalizika mali zao zimekamatwa na tayari kesi zao ziko mahakamani na wangapi wamefungwa.
Katika maoni yao, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii ilisisitiza serikali kuweka utaratibu wa kuwalipa fidia au kifuta machozi kwa wananchi walioathiriwa na operesheni hiyo.
Kuhusu ujangili, Kamati ilishauri kuwa kesi za ujangili zisikilizwe kwa haraka na adhabu kali zinatolewa kwa watakaokutwa na hatia. Aidha, ilishauri serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuwashirikisha wananchi kutatua migogoro ya mipaka kati ya maeneo yanayohifadhiwa na wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo hayo.