VIFARANGA 5,000 vya kuku wa mayai vimekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, vikitaka kuingizwa nchini kwa vibali bandia na vya kughushi vinavyoonesha vilitumika mwaka 2014.

Maofisa wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi walifika uwanjani hapo, ambako ilielezwa kwamba vifaranga hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20, vilikamatwa juzi saa 3 usiku vikitoka Lilongwe nchini Malawi. Vilifikishwa nchini kupitia Nairobi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways). Uchunguzi unafanywa kubaini mmiliki achukuliwe hatua na kuviteketeza.
Katibu Mkuu anayeshughulikia Mifugo katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo alisema jana uwanjani hapo kuwa walipata taarifa siku chache zilizopita kuhusu mzigo huo na kuanza kuufuatilia kwa kushirikiana na maofisa wa Usalama wa uwanja, Mamlaka ya Mapato (TRA) na wizara. "Wameingia bila utaratibu, vibali vimegushiwa.
Mlolongo wa ukaguzi ulianza siku chache zilizopita baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wafugaji wa nchini kuwa kuna vifaranga vinaingia nchini bila kufuata utaratibu," alisema Dk Mashingo. Dk Mashingo alisema baadhi ya vibali, vinaonesha kuwa vilitumika kutoa mzigo kama huo mwaka 2014 na vingine vimeghushiwa kupata mihuri ya wizara.
Alisema vitendo hivyo ni kinyume cha Sheria Namba 17 ya mwaka 2003 ya Kuzuia Magonjwa ya Mifugo na ni ukiukaji wa makubalino ya kimataifa ya kutoingiza vifaranga bila vibali kutokana na kuwapo kwa ugonjwa wa homa kali ya mafua ya ndege. Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara , Dk Abdu Hayghaimo, alisema Serikali ilizuia uingizaji wa vifaranga vya mayai na nyama vya kuku tangu mwaka 2006/2007 kutokana na mafua makali ya ndege.
Serikali iliridhia kuingizwa kwa vifaranga vya uzazi pekee kwa baadhi ya nchi kwa makubaliano ya kimataifa. Alisema yupo mtu kacheza na vibali na saini za watendaji wa wizara kwa kuwa baadhi vinaonesha jina la wizara la zamani (Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na walibaini ni vya zaidi ya miaka mitatu kutokana na namba ya kibali kuonesha ni ya zamani.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, baada ya mzigo kushushwa kwenye ndege, walinzi wa kampuni ya Swissport waliuzuia baada ya kupata shaka. Alisema kifaranga kimoja cha wiki tatu huuzwa kwa Sh 4,000, hivyo hao walioingizwa thamani yake ni Sh milioni 20.
Meneja wa Huduma za Mizigo wa Swissport uwanjani hapo, Wandwi Mugesi alisema walibaini vibali vina utata na vifaranga ni vikubwa, tofauti na vinavyopaswa, ndipo walipozuia mzigo kutolewa uwanjani hapo kusubiri watu wa TRA na wizara kuthibitisha uhalali wa vifaranga hivyo. Kaimu Meneja wa TRA Idara ya Forodha, Julieth Nyomolelo alithibitisha kuwa mzigo huo ulikuwa na vibali vya kughushi.
Alisema ulikuwa umeagizwa na kampuni ya Silifa Company Ltd ya Dar es Salaam. Alisema kampuni hiyo imesajiliwa na kwa kuwa ina namba ya usajili, wanatafuta mmiliki wake. Wakala aliyeingiza mzigo huo kwa niaba ya mmiliki, George Kivelege wa kampuni ya Iralinks Co Ltd, alikiri kusimamia uingizwaji wa mzigo huo nchini .
Alisema yeye aliletewa nyaraka halali zenye mihuri ya wizara na alilipia Mei 25 mzigo ukionesha ni vifaranga vya wazazi vya siku moja. Dk Mashingo alisema watashirikiana na TRA kukagua nyaraka za mizigo mingine ya vifaranga.