WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kila kinachokusanywa kama mapato ya nchi kinatumika kwa maslahi ya Watanzania wote na si kwa manufaa ya wachache. Aidha, amesema watu wanaoamini kuwa uongozi wao na Rais John Magufuli hauwezi kupambana na maovu na kuondoa kero zinazowaumiza wananchi wa kawaida na kwamba utawala wao ni wa watu wapole, waondoe dhana hiyo.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akifunga maadhimisho ya miaka 20 ya Dayosisi ya Pwani ya Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) kwenye Ukumbi wa PTA, Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Serikali imeanza kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma. Nia yetu ni kuhakikisha kila kinachopaswa kukusanywa kama mapato ya nchi, kikusanywe na kitumike kwa masuala ya msingi kwa ustawi wa Watanzania wote na si kwa watu wachache,” alisema Waziri Mkuu.
Akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya Dk Magufuli, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kupambana na maovu yote na kuondoa kero zinazowaumiza wananchi wa kawaida.
“Wako watu wanaoamini kwamba hatuwezi, nawaomba waondoe hiyo dhana. Wako watu wanaodhani kwamba utawala huu ni wa watu wapole, nao pia waondoe hiyo dhana,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya waumini waliohudhuria sherehe hizo zilizoanza Novemba 27, 2015.
“Tunawaomba Watanzania wote mtuunge mkono kwenye vita hii na mtuwezeshe kuifanya kazi hiyo. Tunaomba waumini wote mtuombee katika sala zenu za kila siku ili tuweze kuongoza kwa haki na kuwaletea Watanzania wote maendeleo,” aliongeza.
Akinukuu kitabu cha Mithali sura ya 29 mstari wa pili, Waziri Mkuu alisema: “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi, bali mwovu atawalapo, watu huugua. Mtuombee viongozi wenu tuwe waadilifu na wenye kutenda haki. Nasi tutaendelea kuwa waadilifu ili watu wetu wasiugue.”
Aliwataka viongozi wa kanisa hilo waendelee kuisaidia Serikali katika kujenga kundi la watu wenye maadili mema ili walisaidie Taifa kuwa na watu waadilifu na hivyo kupunguza kero nyingi zinazoikabili jamii.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini waliotoka mikoa mbalimbali, Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT, Askofu Silas Kezakubi alisema Kanisa hilo litaendelea kumuombea Dk Magufuli na viongozi wenzake ili wawe na afya njema, wawe na hekima na kuahidi kwamba wataendelea kuwaweka chini ya ulinzi wa Mungu siku zote.
Alisema wao kama kanisa wanaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ina nia ya kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu, lakini alisisitiza kuwa siri ya bidii na uadilifu inapatikana kwenye neno la Mungu.
Akisoma risala ya kanisa hilo, Askofu wa AICT Dayosisi ya Kibaha, Askofu Charles Salalah alisema kanisa halina budi kushirikiana na Serikali kwa sababu wote wanawahudumia watu walewale isipokuwa katika malengo tofauti.
Alisema kanisa hilo linahubiri maadili mema na bidii katika kazi kwa vile linaamini kuwa maendeleo hayadondoki kutoka juu wala hayaoti kama uyoga bali yanapatikana kwa watu kufanya kazi.
Akisisitiza kuhusu uadilifu, aliwataka wazazi kudumisha ndoa zao ili watoto wapate malezi mema kutoka kwa baba na mama na kwamba baba na mama wasipokaa vizuri, watoto hawawezi kuwa waadilifu. “Wazazi tunao wajibu wa kupanda mbegu bora ya uzalendo kwa watoto wetu. Endapo tutapanda mbegu mbaya ya kuwagawa watoto wetu kwa itikadi tofauti, ni lazima tujue kuwa tutavuna tunachopanda.”
“Tukumbuke kuwa tunalo Taifa moja tu la Tanzania. Hata kama watoto wetu watakuwa na upenzi na vyama vyao, ni lazima tuwalee katika misingi ili wakue wakijua Taifa letu ni moja tu. Ndiyo maana tunaweka mkazo kwenye familia kwa sababu maadili mema yanaanzia nyumbani,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia watumishi wabadhirifu wa fedha za umma, wavivu na wababaishaji. Aliyasema hayo juzi kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sagini katika Mahafali ya Saba ya Chuo cha Serikali za Mitaa kilichopo Hombolo katika Manispaa ya Dodoma.
Aliwataka wahitimu hao kwenda kuwa watumishi waadilifu, wachapakazi wenye tabia nzuri na wenye kutumia utaalamu na weledi waliopata pamoja na nidhamu na matumizi bora ya mali ya umma, ubunifu na kuongeza tija. “Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia kabisa watumishi wabadhirifu wa fedha za umma, wavivu na wababaishaji,” alisema Waziri Mkuu.