UMOJA wa Wazee Wastaafu mkoani Shinyanga (UWASHI), wamempongeza Rais John Magufuli kwa utendaji wake wa kazi ambao wameeleza kuwa unafanana na ule wa enzi ya Mwalimu Julius Nyerere.
Pongezi hizo walizitoa jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ambako walieleza kuwa juhudi za utendaji kazi umejidhihirisha kwa wananchi na umeonekana.

Akizungumza kwa niaba ya wazee, Mkuu wa Wilaya mstaafu Miraji Pazi ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Wazee Wastaafu Mkoa wa Shinyanga, alisema Rais Magufuli tangu aapishwe na kuanza kufanya kazi, amefanya kazi kubwa ambayo imerudisha imani kwa wananchi na imani kwa CCM.
Aidha, aliiomba CCM na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono ili asikwame kuifanya kazi ya serikali waliyomtuma kuifanya, ambapo kwa kuona utendaji wake wa kazi wamekiamini chama kwa kumchagua Rais.
“Kutokana na utendaji wake wa kazi, sisi wazee wastaafu tunamuomba aendelee kuchapa kazi asikate tamaa kwa utendaji wake wa kazi umezidi kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi hivyo kumuunga mkono ili azidi kutumbua majipu yaliyokuwa yanawaumiza watu wengi na kelele za wananchi za kusema mafisadi sasa zimekwisha,” alieleza Pazi.
Pia wazee hao walimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Waziri Mkuu Majaliwa Kassim ambaye kwa mwonekano wake ameonekana ataimudu kazi hiyo kwa sababu ana uzoefu na hana kashfa.
Naye Katibu wa Wazee hao, Mary Mbarakane alisema kutokana na utendaji kazi wa Rais, wafanyakazi na Watanzania wanatakiwa kubadilika, vinginevyo kwa utendaji wake watamchukia Rais ambaye anatenda haki.
Aidha, wazee wastaafu zaidi ya 50 wa mkoa wa Shinyanga walimwomba Rais awakumbuke kwenye shughuli ambazo wana uwezo nazo ikiwemo kutoa ushauri, kwani wana uwezo wa kufanya kazi ndogondogo za muda pia serikali iboreshe maslahi ya wastaafu kwa vitendo