chandeJaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman
Na Hashim Aziz, UWAZI
Dar es Salaam: Matumbo joto! Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli ikiwa kwenye hatua za mwisho za kuikamilisha Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi, tayari mafisadi wameanza kukimbia nchi wakijaribu kukwepa mkono wa sheria, Uwazi limebaini.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu makini, awali Rais Magufuli alipoahidi kuanzisha mahakama hiyo, wengi walichukulia kama ni suala lisilowezekana, lakini kasi yake ya kusimamia suala hilo, imewafanya baadhi ya mafisadi waingiwe na kihoro na kuanza kutafuta njia za kujinusuru ikiwemo kutoroka nchini.
Siku chache zilizopita, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman (pichani) alinukuliwa akisema kwamba kesi zote zitakazofikishwa kwenye mahakama hiyo, zitasikilizwa na kutolewa hukumu ndani ya muda usiozidi miezi tisa na kwamba tayari majaji 14 watakaoanza kusikiliza kesi hizo, wapo kupigwa msasa kwenye Chuo cha Mahakama Lushoto mkoani Tanga.
“Hali ni mbaya, kuna jamaa zangu wanahusika kwenye lile sakata la Escrow (Tegeta Escrow), waliposikia kwamba mahakama ya mafisadi inatarajiwa kuanza kazi muda wowote kuanzia sasa, wametimkia ng’ambo.
“Unafikiri kuna mtu anayependa kupelekwa gerezani? Mmoja amehamishia familia yake Uarabuni na mwingine nasikia amehamia Denmark,” kilisema chanzo hicho na kuongeza kwamba, katika awamu zilizopita, kesi za rushwa na ufisadi mkubwa, zilikuwa zikisikilizwa kwa kusuasua sana ndiyo maana mafisadi walikuwa wakitamba mitaani na wakaongezeka kwa kasi.
Uchunguzi wa Uwazi, umeonesha kwamba vigogo wote ambao kwa namna moja au nyingine walitajwatajwa kwenye kashfa za rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi na  kulisababishia taifa hasara, wameshatimkia nje ya nchi kwa njia za panya na wengine wapo kwenye hatua za mwisho za kuweka mambo sawa kabla ya kutokomea kusikojulikana.
Miongoni mwa kashfa kubwa zilizoitingisha nchi, ambazo vigogo wake wanatarajiwa kuwa wa kwanza kupandishwa kwenye mahakama hiyo ni ya Tegeta Escrow, mabilioni ya Uswisi, malipo ya watumishi hewa na vigogo wa bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB).
Nyingine ni kashfa za Kampuni ya Lugumi Entreprises, vitambulisho vya taifa, makontena yaliyotoroshwa bandarini bila kulipiwa kodi, ununuzi wa mabehewa feki, uingizwaji wa mikataba mibovu na sakata la mashine za stakabadhi za kielektroniki (EFD).