WATU 30 wamefariki dunia baada ya mabasi mawili mali ya Kampuni ya City Boys, kugongana jana asubuhi katika kijiji cha Maweni Tarafa ya Kintinku wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha mabasi aina ya Scania lenye namba za usajili T531 BCE likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama na lingine lenye namba za usajili T247 DCD likitoka Kahama kwenda Dar es Salaam, ambayo yaligongana uso kwa uso. Kwa mujibu wa Kamanda Sedoyeka, waliokufa miongoni mwao ni wanaume 18, wanawake 11 na mtoto mmoja wa kiume.

“Chanzo cha ajali hii kwa mujibu wa majeruhi ni kwamba madereva hao kwa kuwa ni wa mabasi ya aina moja walipokutana hapo wakawa wanachezeana kwa staili ile ya kufanya madoido barabarani hivyo yule aliyekuwa anatoka Dar es Salaam gari likamshinda na kwenda kumgonga mwenzake,” alieleza Kamanda Sedoyeka.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Kamanda Sedoyeka alisema licha ya maelezo hayo ya mashuhuda na majeruhi, wanafanya uchunguzi wa kitaalamu kufahamu kama chanzo ni hitilafu au uzembe kama huo unaosemwa kwamba madereva hao walikuwa wakitaniana na kucheza barabarani.
Aidha, alisema pia haijakuwa wazi kama miongoni mwa waliokufa wamo madereva hao, ingawa taarifa za awali zinadai dereva mmoja amefariki na mwingine ni majeruhi. Kamanda Sedoyeka aliliambia gazeti hili saa 2 usiku jana kuwa maiti watatu wa ajali hiyo wapo Hospitali ya Wilaya ya Manyoni pamoja na majeruhi 48.
Alisema maiti wengine 27 wapo Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Ajali hiyo imetokea takribani siku nne baada ya watu 11 kufa papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea sehemu moja, zikihusisha basi la abiria, lililoparamia malori mawili ya mizigo yaliyogongana uso kwa uso na kuungua moto eneo la Dakawa – Veta wilayani Kilosa, Morogoro.
Rais atuma salamu Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 29 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani, iliyosababishwa na mabasi hayo mawili ya Kampuni moja ya City Boys.
Ametuma salamu zake kwa familia zilizopatwa na msiba huo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe na kuelezea masikitiko yake juu ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya iliyosababisha watu wengi kufariki dunia.
“Nimepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za ajali hii ambayo imesababisha vifo vya idadi kubwa ya Watanzania, kwa hakika nimesikitishwa sana sana na napenda kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. “Namuomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu wanafamilia wote waliopoteza jamaa zao na sote tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, amina,” alieleza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewaombea majeruhi wote wa ajali hiyo, ambao wanapatiwa matibabu hospitali wapate nafuu na kisha kupona haraka ili warejee majumbani kwao kuungana na familia zao katika shughuli za kila siku.