WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa dini, wazazi na viongozi wa serikali kupiga marufuku matumizi ya vilevi aina ya shisha kwamba kinawaingiza vijana kwenye majaribu na kuharibu maadili kwenye jamii.
Amesema tamko lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda sio kutoka kichwani mwake, bali ni agizo la serikali na kwamba viongozi wote wa mikoa na wilaya na mameya wanatakiwa kukemea suala hilo.

Alisema hayo Dar es Salaam juzi katika futari iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Shia Ithna-Asheri, iliyofanyika kwenye msikiti uliopo Mtaa wa Indira Gandhi, iliyokutanisha viongozi mbalimbali wa dini na serikali.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema watakaokaidi agizo hilo pamoja na wauzaji wa vilevi hivyo, watachukuliwa adhabu kali kwa kuwa wazazi na serikali kwa ujumla wana uwezo wa kudhibiti tatizo hilo.
Alisema viongozi wengine wanatakiwa kuunga mkono tamko hilo na kusisitiza kwamba shisha inaharibu nguvu kazi ya Taifa, kwa kuwa inaondoa vijana wenye uwezo kimwili na kiakili ambao wanaweza kufanya kazi. “Nimeambiwa nitoe tamko kama serikali juu ya matumizi ya tumbaku inayoitwa shisha.
Hii ina mchanganyiko mwingi ambao huvutwa na kutoa moshi mwingi, maji yake huwekwa gongo na vilevi mbalimbali hivyo mvutaji hupata ladha mbalimbali ambazo siku akikosa hutafuta mahali popote,’’ alisema Majaliwa.
Alisisitiza kuwa viongozi wa dini wanatakiwa kutumia nyumba za ibada, kukemea matendo hayo ambayo yanasababisha kufanyika kwa uovu pamoja na kuharibu maadili katika jamii.
Aidha, waziri huyo amewataka viongozi wa dini kote nchini, kutumia nyumba za ibada kuzungumzia amani, upendo na uvumilivu ili kujenga jamii yenye maelewano na ushirikiano.
Alisema serikali itaendelea kuunga mkono na kuheshimu michango mbalimbali inayowasilishwa na viongozi wa dini kwani wanaamini kwa kupitia wao taifa litabadilika.
“Viongozi wa dini mkihimiza waumini wenu kumcha Mwenyezi Mungu, taifa litakuwa bora na lenye utiifu katika kutekeleza mambo mbalimbali ya serikali, hivyo serikali imeamua kusimamia kwa dhati maadili na viongozi watumikie wenzao kwa kuwa na maadili mema na uaminifu,’’ alisema.
Alisisitiza uvumilivu ni jambo nyeti, kwani Watanzania watapata faida kubwa kwa kuwa asilimia 70 ya wafanyabiashara waliopo nchini wanafanya biashara yao kwa amani na utulivu bila ya bughudha yoyote.
Alisema serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwataka waendelee kuimarisha kamati za amani katika ngazi ya mikoa na wilaya kwani kamati hizo zinazojumuisha dini zote zinasaidia kuwaunganisha kwa kukaa pamoja bila mashaka yoyote; inadhihirisha kuwa wako pamoja kuelezea kuhusu amani.
Kwa mujibu wa Majaliwa, serikali inaheshimu dini zote jukumu lao ni kujenga mazingira mazuri kwa kila Mtanzania kushiriki kwa uhuru kwenye dini yake na kuwa na mshikamano. Aidha, alisema dini zimejikita kuisaidia serikali ikiwemo huduma za jamii kwa kujenga shule za elimu ya awali hadi vyuo, kutoa huduma za afya kwa kujenga zahanati na hospitali.
Pia alisema viongozi hao wanahamasisha kilimo kwa kuwapa vifaa na vitendea kazi kwa kuwa ndio umuhimu wa kuwepo na dini.
“Nimepokea madawati 1,000 kutoka jumuiya hizi, tulipozungumzia elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari lengo ni kuwapunguzia wazazi mzigo wa kuwapeleka watoto shuleni kwa sababu tuliona kuwa wapo watoto wengi ambao walikuwa wanakaa majumbani bila ya kwenda kusoma kutokana na kushindwa kulipiwa ada,’’ alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhamasisha amani na kuheshimiana baina ya mtu na mtu.
Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema watahakikisha kwamba wanaunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo katika nchi, kulinda amani na uchumi kwa nchi.