Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze
ASILIMIA 42 ya Watanzania wamesema njia sahihi ya kushughulikia mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar ni kumtambua Rais Ali Mohamed Shein aliyechaguliwa kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi mwaka huu kama rais halali.

Aidha, asilimia 14 wanataka aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad atangazwe kama mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka jana.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze wakati akitangaza kwa waandishi wa habari matokeo ya utafiti waliofanya.
Utafiti huo uliohusu Masuala ya Muungano: Maoni ya wananchi kuhusu kinachoendelea Zanzibar na ulilenga kupata mtazamo wa wananchi wa Tanzania Bara juu ya kinachoendelea Zanzibar.
Kwa mujibu wa Eyakuze, matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kwa simu kutoka kwa wahojiwa 1,815 wa maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara kati ya Machi 29 na Aprili 12, mwaka huu. Eyakuze alisema asilimia 20 ya wananchi wa Tanzania Bara walisema uchaguzi wa marudio ulikuwa ni hatua nzuri ya kutatua mgogoro.
Asilimia 13 wametaka kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kumaliza mgogoro huo huku asilimia nane wakiwataka viongozi wa siasa kumaliza tofauti zao kwa majadiliano.
Wakubaliana matokeo kufutwa Akizungumzia kuhusu utafiti uliofanyika katika eneo la ufutwaji wa matokeo, Eyakuze alisema wananchi sita kati ya 10 sawa na asilimia 59, walikubaliana na ufutwaji wa matokeo huku asilimia 40 wakipinga.
“Wananchi asilimia 60 walikubali Zanzibar kufanya uchaguzi wa marudio lakini asilimia 39 wamekataa kurudiwa kwa uchaguzi mpya, lakini pia asilimia 60 ya wananchi wamekataa vyama vya upinzani kususia uchaguzi na asilimia 39 wao walikubali,” alifafanua Eyakuze.
Akizungumzia kuhusu mtazamo wa wananchi juu ya kinachoendelea Zanzibar, Eyakuze alisema pamoja na visiwa hivyo kukumbwa na matukio mengi wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu ikiwemo viongozi wa vyama vya upinzani na wafuasi wao kugoma kushiriki uchaguzi wa marudio, lakini asilimia 53 ya Watanzania Bara wamesema hawafahamu kilichojiri Zanzibar tangu ulipofanyika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana.
Aidha, wananchi wanne kati 10 waliohojiwa ambao ni sawa na asilimia 20 walisema wana taarifa kuwa uchaguzi ulifanyika Machi 20, mwaka huu. Asilimia 18 walifahamu matokeo ya uchaguzi wa Oktoba yalifutwa, asilimia nane walifahamu upinzani kugomea uchaguzi wa marudio na asilimia 0.5 walifahamu kulitokea na vurugu.
“Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi zina kazi kubwa ya kurejesha umoja baina ya wapiga kura wa visiwani Zanzibar. Lakini inatia wasiwasi kubaini kuwa idadi kubwa ya Watanzania walikiri kutojua kilichotokea visiwani Zanzibar baada ya uchaguzi wa Oktoba 25. “Hali hii inaudhoofisha Muungano wetu, tukitaka kudumisha muungano wetu hatuna budi kama wananchi kufuatilia kwa karibu sana,” alisema mtendaji huyo wa Twaweza.