Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi
WAKURUGENZI wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya walioteuliwa Jumatano ya wiki hii, wametakiwa kuwasilisha nakala halisi za vyeti vyao vya taaluma, kabla ya kuapa.
Wakurugenzi hao wa majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137 nchi nzima, wanatarajiwa kuapishwa Ikulu Dar es Salaam keshokutwa.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, imewataka wakurugenzi hao kuwa watakapofika kwa ajili ya kiapo cha uadilifu wa uongozi wa umma, wahakikishe wanafika na nakala zao halisi za vyeti vya kitaaluma kwa ajili ya ukaguzi.
“Ieleweke kuwa uhakiki wa vyeti halisi vya kitaaluma, unafanywa kwa lengo la kujiridhisha baada ya mchakato wa kawaida wa uhakiki kufanywa kwa kutumia vyeti visivyokuwa halisi yaani vivuli,” imeeleza taarifa hiyo iliyotumwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Taarifa hiyo imesema kuwa uhakiki huo wa vyeti utaanza saa mbili asubuhi na kuwataka wahusika wote kuingia Ikulu kwa kupitia geti kuu lililopo upande wa Mashariki, linalotazamana na bahari ya Hindi. Hatua hiyo ya Ikulu imekuja wakati taifa likikabiliwa na changamoto ya kukithiri kwa udanganyifu katika vyeti wakati wa kuomba ajira.
Takwimu za mwaka juzi zilionesha kuwa ndani ya mwaka huo, watumishi 1,360 walikutwa na vyeti visivyo halali. Uhakiki wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) katika mwaka huo, ulibaini kuwa baadhi ya watumishi wakiwemo wa serikali walikutwa wakitumia vyeti vya kughushi ambavyo vimebadilishwa matokeo, wengine walikutwa na vyeti vya bandia huku wengine wakitumia vyeti vya watu wengine.
Mwaka huo huo, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ilitoa taarifa ikieleza kubaini kuwepo kwa udanganyifu wa vyeti 677, kwa watumishi serikalini.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya watu 13,554 walioomba ajira katika miaka mitatu yaani 2010, 2011 na 2012; watu 816 walibainika kudanganya kwa kutumia vyeti vya taasisi mbalimbali za elimu, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.
Kutokana na hali hiyo, Necta ilitangaza kuanza kujipanga kushirikiana kwa karibu na mamlaka za ajira na udahili, ili kuhakikisha uhakiki wa vyeti vinavyotolewa na baraza hilo, unafanyika kabla ya mtahiniwa kuajiriwa au kudahiliwa.