Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Aug 26, 2016

Amani kwanza


Rais John Magufuli
VIONGOZI wastaafu, vyama vya siasa, wanaharakati wa masuala ya sheria na wanawake viongozi katika vyama vya siasa wamehubiri suala la amani wakati huu ambao kumekuwapo na sintofahamu ya kisiasa kutokana na hatua mojawapo ya chama cha siasa nchini kutangaza maandamano yasiyo na kikomo.
Kwa siku kadhaa sasa, kumekuwa na hofu miongoni mwa jamii kuhusu hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza Operesheni ya Kuzuia Udikteta Uchwara Tanzania (Ukuta) ambayo itakwenda sambamba na maandamano nchini, ambayo hata hivyo yamepingwa na viongozi wakuu wa kitaifa na Jeshi la Polisi.

Rais John Magufuli alitangaza marufuku ya maandamano hayo yasiyo na ukomo na kutaka wanasiasa wafanye kazi za maendeleo katika majimbo yao, huku Jeshi la Polisi likizuia mikutano yote ya ndani na nje yenye nia ya kuleta uvunjifu wa amani.
Aidha, akiwa Sumbawanga wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.
“Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.
Kutokana na hilo, viongozi mbalimbali nchini wakiwamo wastaafu wamezungumzia suala la kutanguliza amani kwanza na kutaka kuwapo kwa mazungumzo yenye nia ya kufikia mwafaka wa hali ya kisiasa iliyopo nchini kwa sasa.
Warioba, Lowassa
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu alisema viongozi wakuu wastaafu ambao ni marais na mawaziri wakuu wamekuwa wakimshauri Rais katika masuala mbalimbali.
“Kweli tuko kimya lakini ukimya huo usitafsiriwe kuwa hatumshauri Rais sisi kama viongozi wastaafu, lakini haifanyiki kwenye vyombo vya habari,” alisema Jaji Warioba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Kingunge Ngombale-Mwiru aliwataka viongozi wote wastaafu nchini wakiwemo marais na mawaziri wakuu kuingilia mvutano wa kisiasa unaoendelea sasa kuhusu Ukuta kutafuta muafaka.
Jaji Warioba alisema badala ya kumjibu Kingunge ni vyema kumuachia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi awakutanishe viongozi wa vyama vya siasa kujadili hali hiyo kwa lengo la kupata muafaka.
Hata hivyo, alisema ni wajibu wa Watanzania wote kuhakikisha wanalinda hali ya amani nchini badala ya kuliona jambo hilo linamhusu Rais John Magufuli pekee au mtu mwingine yeyote. “Tumsaidie msajili katika hili, hili sio tatizo la mtu mmoja bali ni la nchi nzima tusimuachie Rais,” alisema Jaji Warioba.
Aidha, alisema jambo ambalo linafanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa la kuandaa majadiliano ni jambo jema zaidi na kwamba yakifanyika mambo mengine yanaweza kuleta madhara kwa wananchi.
Jaji Mutungi hivi karibuni alipozungumza na vyombo vya habari aliwatoa hofu wananchi kuwa hakutakuwa na uvunjifu wa amani kutokana na sintofahamu inayoendelea nchini baina ya vyama vya siasa.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alipozungumza na gazeti hili jana alisema mazungumzo ni jambo zuri kuliko maandamano. Lowassa alisema ushauri wa Kingunge wa viongozi wastaafu kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kwa lengo la kumshauri juu ya hali ya kisiasa inavyokwenda ni wa busara.
“Ushauri wa Mzee Kingunge ni wa busara sana na mimi naona viongozi wa zamani tukae tufanye mazungumzo na Rais kuliko kufanya maandamano,” alisema Lowassa.
Cleopa Msuya
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya alisema serikali imetoa mwongozo wake watu wauzingatie na siyo kufanyika mazungumzo.
Alisema viongozi wa vyama vya upinzani waliotangaza operesheni hiyo kama wana hoja za msingi waseme ili zipatiwe ufumbuzi, lakini siyo kuvunja miongozo iliyowekwa makusudi.
“Tukae tuzungumze na Rais tunazungumza nini? Kama una watoto wako umeweka miongozo wengine hawataki kufuata mnazungumza? Kama wana tatizo waseme kuna moja, mbili, tatu, sasa waache wapambane na dola,” alisema Msuya na kuongeza kuwa Rais Magufuli anatosha, aachwe afanye kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na watu wengine.
Kwa upande wao, Umoja wa Viongozi Wanawake wa vyama vya siasa nchini wamepinga harakati za kisiasa zenye mrengo wa kuhatarisha maisha na kuchochea vurugu.
Katibu wa Umoja huo, Mwajuma Noty alisema pamoja na kupinga harakati hizo, viongozi hao pia wanapinga azimio la maandamano yasiyo na kikomo yanayoandaliwa na Chadema kwani maandamano hayo hayana tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Matukio yanayojitokeza hivi sasa sisi wanawake tunaona hali hiyo inaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi, chokochoko hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila kukemewa tunaamini tunu yetu ya amani ambayo ni urithi tulioachiwa na waasisi wetu itatoweka,” alisema Noty.
Aliongeza kuwa hatma ya yote hayo ni kuingia kwenye machafuko ambayo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu watateseka kwa kufanywa vilema na kuuawa.
“Hatutakubali hili litokee, tunaamini siasa ni kushindana kwa hoja na sio uvunjifu wa sheria kwa njia ya maandamano yasiyo na maslahi kwa wananchi na taifa,” aliongeza na kumwomba Rais Magufuli kuona namna nzuri ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa kisiasa.
Bisimba wa LHCR, Mbatia, Mwakyembe
Aidha, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimevishauri vyama vya siasa nchini kushindana kwa hoja na kuacha kutumia vyombo vya dola katika kushinikiza hoja au matakwa yao, jambo litakalosaidia kuimarisha haki za binadamu na demokrasia nchini na kusaidia kuleta usawa na ushindani wa kweli miongoni mwa vyama hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba wakati akizungumzia hali ya haki za kiraia na kisiasa nchini huku pia akilaani tukio la mauaji ya askari Polisi yaliyotokea katika eneo la Mbande, alisema kama vyama vya siasa vikishindana kwa hoja, itakuwa ni fursa kwa wananchi na Watanzania kusikia, kuelewa na kupambanua hoja na kujenga jamii yenye uelewa na upeo mpana kuhusu masuala yanayowahusu ya ndani na nje ya nchi.
Nao Umoja wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa) umewaomba viongozi wa dini nchini kuendeleza kasi ya kuomba Rais afanye meza ya mazungumzo kwa sababu ndio njia pekee itakayoleta maridhiano nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati viongozi mbalimbali wa vyama vinavyounda Ukawa pamoja na Chama cha ACT-Wazalendo, wakizungumza na waandishi wa habari.
Mbatia aliyekuwa akitoa mrejesho wa mkutano uliofanywa hapo juzi baina ya vyama vya siasa nchini na viongozi mbalimbali wa dini kuhusu hali ya siasa, alisema viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha amani ya nchi inalindwa na kwamba jitihada hizo zimesaidia kuifanya nchi ikatulia.
“Tunawashukuru sana viongozi wa dini wanajitahidi sana kusaidia nchi ikasonga, na tunashukuru tunaomba watakapozungumza na Rais John Magufuli wazungumzie meza ya maridhiano kwa sababu ndiyo ustaarabu wa kuendesha nchi duniani kote, na ndio njia pekee itakayotusaidia sasa,” alisema Mbatia.
Akizungumzia rai ya viongozi wa dini kuhusu vyama hivyo vinne vilivyosusia vikao vya Bunge, Mbatia alisema wamepokea mwito wa viongozi wa dini wa kuvitaka vyama hivyo kurejea bungeni huku wakiangalia njia nzuri zaidi ya kutafuta suluhu.
“Ni kweli viongozi wa dini tulifanya nao kikao hapo jana (juzi) na tumepokea rai yao na vyama vinavyounda Ukawa tutakutana na kuzungumzia rai hiyo ili tuangalie jinsi ya kutekeleza kwa maslahi ya Tanzania na sio mtu binafsi”, alisema Mbatia.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya nje na ndani ya vyama vya siasa ni halali ambayo kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote cha siasa anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.
“Jeshi la Polisi ni chombo halali cha dola kilichoanzishwa kisheria chenye wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuongeza kuwa uamuzi huo una lengo la kulinda amani ya nchi na endapo kutakuwa na viashiria vya kutishia amani ya nchi yetu lazima hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe,” alisema Dk Mwakyembe akijibu swali la waandishi wa TBC1 jana.
“Ni amri halali na kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote nchini anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kwenda kinyume ni kukiuka sheria.”
Imeandikwa na Regina Kumba, Lucy Lyatuu, Sophia Mwambe na Ikunda Erick.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP