Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson
Lwenge akifungua  kikao cha pamoja na
ujumbe wa Benki ya dunia, Wizara ya Maji ,Shirika la Majisafi na Majitaka
jijini Dar es Salaam (Dawasco ) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar
es Salaam (Dawasa) namna ya kutatua changamoto za usambaza Maji kwenye Jiji la
Dar es Salaam yakiwamo Mivujo na Miundombinu chavu , kilichofanyika Jijini Dar
es salaam.


Dar es Salaam.



KATIKA
kuhakikisha sekta ya Maji inakua kwa kasi na inatosheleza mahitaji ya sasa ya
huduma ya maji, Benki ya Dunia imejitolea kulisaidia Shirika la Majisafi na Majitaka
jijini Dar es salaam (DAWASCO), ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma ya
Majisafi na Majitaka katika maeneo mbalimbali ya wakazi wa jiji la Dar es
salaam pamoja na Miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.


Hayo
yamezungumzwa na Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bi. Bella Bird, ambaye
alikuwa ameambatana na wajumbe wake katika kikao cha pamoja na Waziri wa Maji,
Mhandisi Gerson Lwenge, pamoja na Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es
Salaam (DAWASCO). 


Kikao ambacho kililenga uboreshaji na upatikanaji wa huduma
ya Maji katika maeneo kadhaa ya jijini Dar es Salaam hasa maeneo ambayo
hayajafikiwa na huduma hiyo.


Aidha,
Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia, ameridhishwa na juhudi za makusudi
zinazofanywa na Dawasco katika kuwapatia wananchi huduma ya Majisafi, pamoja na
kupambana na kiwango cha Maji kinachopotea bila sababu ya msingi. 


Ameeleza
kuwa Benki ya dunia imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Majisafi
na Majitaka ili kuimarisha uendeshaji wa utoaji wa huduma ya Maji kwa wananchi,
ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu kampeni ya “Mama Tua Ndoo Kichwani” ili kuwapunguzia akina mama wengi tatizo la
Maji, kwani ndio wanaoonekana kuwa wahanga wakuu wa tatizo hilo.


Nimeridhishwa
na utendaji wenu wa kazi, jinsi ambavyo mmejipanga katika kufanya kazi, hasa
juhudi zenu mnazoziweka katika kupambana na upotevu wa Maji na kuwapatia
wananchi huduma ya Maji” alisema Bi.
Bird


Naye,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru Benki ya
Dunia kwa ushirikiano mzuri waliouonesha, na kwamba kiasi cha fedha
kilichotengwa na Benki ya Dunia kitatumika katika kuboresha na kutatua
changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika katika utoaji wa huduma ya Maji.


Changamoto
ni nyingi katika utoaji wa huduma ya Maji, naamini kuwa kiasi cha fedha
kilichotengwa kitasaidia kuondoa changamoto hizo” alisema Mhandisi Luhemeja.


Benki
ya dunia imekuwa ikifadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwamo
miradi mbalimbali katika sekta ya Maji, Nishati na Madini, Kilimo na Mifugo,
pamoja na Uchumi na Biashara.