Donald Trump amewalaumu waandishi wa habari baada yake kushutumiwa kwa matamshi yake ambapo alidaiwa kuwahimiza wafuasi wake wamuue mpinzani wake Hillary Clinton wa chama cha Democratic.
Alikuwa amewaambia wafuasi wake kuwa wanaweza kumzuia hasimu wake Bi Clinton kwa kutekeleza haki zao za silaha.

Alisema Bi Clinton anaweza kupeleka haki zake huria za kisheria mbele ya Mahakama ya Juu kama atashinda urais mwezi Novemba, na kufuta haki ya raia kumiliki silaha.
Akihutubia mkutano wa kisiasa katika jimbo la North Carolina, Bw Trump alidokeza kuwa haki za umiliki wa silaha zinaweza kusaidia kumzuia Bi Clinton kuchukua mamlaka.
Kauli yake hiyo imezua hasira kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimshutumu kwa kuchochea ghasia.
Lakini muda mfupi baadaye alijitetea na kusema kuwa alikuwa tu anawataka wanaounga mkono haki za umiliki wa silaha kupiga kura kwa wingi.
Baadaye alisema wanahabari wa shirika la habari la Fox News walipinda matamshi yake na kuyafanya yaonekane kana kwamba alikuwa anawahimiza wafuasi wake wenye silaha wazitumie kumuangamiza Bi Clinton.
Hii si mara ya kwanza kwa Bw Trump kulazimika kukosoa kauli zake.

1. Kumbeza mlemavu

Aliwahi kukanusha kumbeza mwandishi wa habari mlemavu wa gazeti la New York Times Bw Trump alilegeza mikono yake alipokua akielezea makala kuhusu mashambulizi ya 9/11 iliyoandikwa na Serge Kovaleski, ambae ana ulemavu wa mikono. Hata hivyo mwanasiasa huyo alisistiza kuwa hakujua ripota huyo anafanana vipi na kwamba anawaheshimu watu wenye ulemavu.

2. Iran kulipwa pesa

Donald Trump aliwahi kufafanua baada ya awali kudai kuwa aliona mkanda wa video wa malipo ya pesa ya Marekani kwa Iran. Alitoa madai hayo kwenye mkutano wa kisiasa. Trump alisema malipo yalikua na uhusiano na Iran kukubali mapatano ya nyuklia

3. Wanawake kutoa mimba

Donald Trump alifuta kauli yake ya awali ambapo alisema wanawake waliotoa mimba waadhibiwe saa chache tu baada ya kutoa pendekezo hilo. Alipendekeza kuwa "aina fulani ya adhabu " itolewe kwa wanawake waliotoa mimba kama zitakuwa kinyume cha sheria. Lakini baada ya ukosoaji mkubwa , Bw Trump akarejelea msimamo wa chama cha Republican kwamba mtu anaefanya kitendo cha utoaji mimba anapaswa kuadhibiwa, si mwanamke pekee.

4. Kudukuliwa kwa Clinton

Donald Trump alisema alitumia tu lugha ya mzaha alipokowaalika warusi wadukue jumbe za Bi Hillary Clinton zilizopotea. Aliikiambia kituo cha televisheni cha Fox News kwamba chama cha Democrat kilikua tu kinatumia mzozo huo kukwepa masuala makuu. Kauli zake zilikua kuhusu jumbe 30,000 za barua pepe za Bi Clinton ambazo hakuziwasilisha kama sehemu ya uchunguzi kuhusu jumbe za siri. "nilikua najaribu kuwa mzushi tu," Bw Trump alikiambia kituo cha Fox News.