Aliyekuwa kiongozi kwa muda mrefu nchini Cuban Fidel Castro amewashukuru wafuasi wake kwa kumtakia heri akitimiza umri wa miaka 90.
Kwenye barua iliyochapishwa kwenye gazeti la chama tawala cha kikomunisti nchini humo, amesimulia kumbukumbu za maisha yake ya ujana.
Baadaye, amezisifu Uchina na Urusi lakini akamshutumu Rais wa Marekani Barack Obama.
Fidel Castro alitawala Cuba kwa zaidi ya miaka hamsini kabla ya kumkabidhi nduguye Raul madaraka.
Raul Castro ameleza mengi ya masharti ya kiuchumi yaliyokuwa yamewekwa chini ya utawala wa Fidel na pia akafufua uhusiano na Marekani.
Fidel Castro hajaonekana hadharani kwa miezi kadha.
Mwezi Machi baada ya Rais Obama kuzuru Cuba, Fidel Castro pia alimshutumu vikali.
Kwenye barua iliyochapishwa katika gazeti la serikali ya nchi hiyo la Granma, Bw Castro alisema Cuba haihitaji zawadi zozote kutoka kwa Marekani.

'Mshtuko wa moyo'


Fidel Castro kwenye picha iliyopigwa 2006Image copyrightGETTY IMAGES
Image captionCastro amewahi kusema kwamba hakuzaliwa akiwa mwanasiasa

Akijibu pendekezo la Bw Obama kwamba wakati umefika wa kuunda urafiki na kuzika kwenye kaburi la sahau masalio ya Vita Baridi bara Amerika, Fidel Castro aliwakumbusha wasomaji kuhusu uvamizi wa Bay of Pigs uliofanywa na wakimbizi wa Cuba wakisaidiwa na Marekani mwaka 1961.
Alisema maneno ya Obama ya kuhimiza maridhiano ni sawa na "rojo ya sukari" na kuonya kwamba raia wa Cuba wanaweza kupata "mshtuko wa moyo".
Fidel Castro, 89, aliongoza Cuba kuanzia 1959 hadi 2008 alipomkabidhi nduguye madaraka.