RAIS John Magufuli ambaye pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana alikutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Balozi Liberat Mfumukeko na kumsihi ahakikishe Jumuiya inajielekeza kukabiliana na matatizo ya wananchi na kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.

Alisema ni vyema jumuiya hiyo itilie mkazo katika kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na matatizo muhimu ya wananchi yakiwemo upatikanaji wa maji, uboreshaji wa miundombinu kama vile barabara na reli, kuimarisha huduma za afya, kujenga viwanda vitakavyozalisha ajira na kuongeza mapato na kukuza biashara na uwekezaji.
“Itakuwa ni manufaa zaidi endapo nyie watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mtafanya juhudi kubwa kuhakikisha nchi wanachama zinajikita kukabiliana na matatizo ya wananchi, mkifanya hivyo na mkaepuka matumizi makubwa ya fedha kwenye mambo yasiyo ya lazima tutanufaika zaidi,” alisema Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam jana.
Aidha, amempongeza Katibu Mkuu huyo aliyeshika wadhifa huo kuanzia Aprili mwaka huu kwa mipango na mikakati mizuri aliyoanza nayo katika kutekeleza malengo ya Jumuiya ikiwemo kupunguza matumizi, kuvutia wawekezaji na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi na programu iliyo chini ya jumuiya hiyo.
Balozi Mfumukeko pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwake, ameahidi kutekeleza wajibu wake vizuri na kwa manufaa ya wana Afrika Mashariki.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu (UNFPA) nchini, Dk Natalia Kanen aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA.
Amempongeza kwa kuteuliwa kwake na amesema anaamini atakuwa balozi mzuri wa Tanzania hususan katika kuongeza mkazo kwa Umoja wa Mataifa kuisaidia nchi kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ongezeko la wakimbizi, umasikini na huduma za mama na mtoto.