Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa
TUKIO la kujilipua kwa mafuta ya petroli na kisha kujiwasha moto kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Shule ya Sekondari Merinyo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Romanus Shirima (74) limeleta sintofahamu kutokana na mazingira ya kifo hicho kuwa ya kutatanisha.

Tukio hilo ambalo limeacha maswali mengi kwa wakazi wa mji wa Moshi na viunga vyake, lilitokea Agosti 18, mwaka huu saa 11:25 alfajiri nyumbani kwake eneo la Mjohoroni Kata ya Msaranga Ng’ambo katika Manispaa ya Moshi.
Gazeti hili lilifunga safari hadi eneo la tukio, ambako baadhi ya majirani walisema hadi sasa imekuwa vigumu kuamini tukio lililotokea kutokana na mahusiano mazuri, aliyokuwa nayo mzee huyo na majirani.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Shirima, alisema tukio hilo limeacha wananchi wengi midomo wazi kutokana na maamuzi magumu, yaliyofanywa na mwenzao ambaye ilieleza kuwa alikuwa mstari wa mbele kanisani (mzee wa dini) na alikuwa anaketi kiti cha mbele katika ibada.
Jirani mwingine alijitambulisha kwa jina la Mama Nyama, alisema mfanyabiashara huyo alifika katika eneo lake la biashara akiwa na binti yake anayeishi nchini China, na kumletea zawadi ya magazeti pamoja na kumtambulisha kwa binti yake huyo.
Alisema alikuwa mtu mpole na mtaratibu, na ilikuwa vigumu kugundua mambo yake, ndio maana uamuzi aliouchukua umekuwa mgumu kutokana na kutoacha ujumbe wowote ule, unaoashiria sababu za tukio hilo.
Mama Nyama alisema jana walifanya misa ya jumuiya nyumbani kwa marehemu ; na juzi pia walisali misa ya kumuombea katika Kanisa la Katoliki la Kristo Mfalme Jimbo la Moshi Mjini, ambako viongozi wa kanisa walisema suala hilo sio la kawaida wala kujitakia, hivyo watatoa ushirikiano katika mazishi.
“Tunashindwa kuamini tukio hili kwa sababu mzee alikuwa mstari wa mbele katika kunishinikiza kufanya ibada kila mara na kumtegemea Mungu, nilipokuwa napatwa na majaribu ya watoto wangu, hususani kipindi walipokuwa wanafaulu huku nikiwa sina fedha, kila siku mzee aliniambia piga magoti na uombe hakuna linaloshindikana kwa Mungu, sasa nashindwa kuelewa nini kimemsibu,” alisema Mama Nyama.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, mkuu mmoja wa Shule ya Sekondari iliyopo mjini Moshi, alisema Mzee Shirima alifika shuleni kwake siku moja kabla ya kifo chake, ambako alienda kuomba ushauri namna ya kupata idadi kubwa ya wanafunzi katika shule yake ya Merinyo.
Gazeti hili lilifika katika Shule ya Sekondari Merinyo iliyokuwa inamilikiwa na mfanyabiashara huyo, ambako lilishudia idadi ndogo ya wanafunzi wakiwa katika makundi wakijisomea. Mlinzi wa shule alikataa kuzungumzia jambo lolote, ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano wa kuonana na mwalimu na mwanafunzi yeyote.
Mmoja wa mabinti wa marehemu, Rosepilsin Shirima, alisema familia haipo tayari kuzungumzia suala hilo, kwani bado wapo kwenye mshtuko, na hawajui nini chanzo cha baba yao kuchukua uamuzi huo.
Alieleza kuwa maziko, yatafanyika keshokuwa Jumanne wilayani Rombo.
“Hatuwezi kuzungumzia mambo haya kwa sasa, familia nzima ina mshtuko wa tukio hili, baba yetu ametulea vizuri sana tena kwa upendo, tumeishi naye vizuri, ila kwa sasa naomba mtuache kwanza,” alisema Rosepilsin ambaye baba yake alikuwa akimiliki sekondari ya Merinyo, yenye kidato cha kwanza hadi cha nne. Ni shule ya bweni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa alisema bado wanaendelea na uchunguzi, lakini hadi sasa hakuna taarifa wala kiashiria chochote kinachohusu tukio hilo.
Kamanda Mutafungwa alisema taarifa walizozipata kutoka kwa mkewe marehemu, zinasema siku ya tukio Agosti 18, saa 11:25 alfajiri mumewe alitoka nje bila kumtaarifu mtu yeyote na kwenda uwani, lilipo shamba lao la majani.
Kamanda alisema kwa mujibu wa taarifa za mke huyo, muda huo ulikuwa wa kufanya sala ya asubuhi, ambapo baada ya kuamka na kumsubiri mumewe bila mafanikio, alitoka nje na ndipo alipona geti la uwani lipo wazi.
Mutafungwa alisema mke wa marehemu, akiwa katika geti la uwani lililokuwa wazi, aliona moshi mkubwa ukifuka katikati ya shamba lao la mahindi, na baada ya kwenda kushuhudia, alikuta ni mumewe akiwa amekwishateketea kwa moto.