Rais John Magufuli akihutubia maelfu ya wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mkutano uliofanyika Viwanja vya Furahisha, Kirumba jijini humo jana. (Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mwanza, kuhakikisha kuwa watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU), wanapatikana na kuzirudisha mali hizo mara moja, huku akiitaja Kampuni ya Simon Group yenye umiliki katika kampuni za UDA na mabasi ya haraka Dar es Salaam (UDA-RT).

Amesema NCU kwa sasa inashindwa kujiendesha kutokana na watu wachache kujitwalia mali za NCU kwa kuzinunua kwa bei ya hasara, kiasi cha kuifanya NCU kutokuwa na uwezo wa kununua mazao ya wakulima.
“RC (mkuu wa mkoa) umezungumza kwamba katika miaka yote aliyepewa alikuwa anunue kwa bilioni moja pointi amelipa milioni 30 tu na nasikia ni Simon Group. Mimi ni msemakweli na wala sitaki kuzunguka sijui nikasemee wapi,” alisema Rais Magufuli akiitaja kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara Simon Kisena.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha vilivyopo Manispaa ya Ilemela.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alimshukuru Rais Magufuli licha ya kuwa na ratiba ngumu ya kikazi, lakini ameonesha mapenzi makubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili.
Alisema mkoa umeanza na juhudi ya kufufua zao la pamba sanjari na kuanza kurudisha mali za NCU, ambazo ziliporwa na baadhi ya watu, alimuomba Rais Magufuli kuisaidia Serikali ya Mkoa ili kuhakikisha watu wote waliopora mali za NCU wanazirudisha kwa wakulima na wafikishwe mahakamani.
Lakini Rais Magufuli katika hotuba yake, alisema NCU kwa sasa inashindwa kujiendesha kutokana na watu wachache kujitwalia mali zake kwa kuzinunua kwa bei ya hasara, kiasi cha kuifanya kutokuwa na uwezo wa kununua mazao ya wakulima.
“Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma. Waziri wa Ushirika, ni heri ukose kula, mimi nitakuchagua kwenye viti maalumu, lakini mali za Nyanza zirudi,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka mafisadi wakae chonjo kuwa tayari kufikishwa mahakamani kwa sababu Bunge tayari limeishaipitisha sheria hiyo, ambayo itaanza utekelezaji wake mara moja.
Alisema sheria hiyo itakuwa ni mkombozi wa Watanzania ambao hivi sasa wamechoka na rushwa, ambapo alikiri kuwa kwa sasa rushwa ipo kila mahali nchini.
“Nawashukuru sana wabunge (hasa wa CCM) kwa kupitisha sheria hiyo ya mafisadi,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu uvuvi haramu kwa kutumia zana zisizokubalika kisheria, Rais Magufuli alishangaa kuona vyombo vilivyopewa jukumu la kudhibiti hali hiyo vikizembea wakati uharamia huo ukiendelea.
“Kama kuna mtu alichoma makokoro ni mimi na samaki waliongezeka. Wanapita kuna Polisi, Uhamiaji, TRA, lazima tulinde rasilimali yetu ili Watanzania waweze kufaidika. Hizo zana zinapitishwa kwenye mipaka, shikeni na hilo gari mtaifishe moja kwa moja kwa sababu hayapiti angani,” alieleza.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba hakuna aliyeshinda wala kushindwa, bali Watanzania wote wameshinda. Alisisitiza kuwa atatekeleza ahadi zote alizoahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu ikiwamo kulifanya Jiji la Mwanza kuwa jiji la biashara.
Akizungumzia hatua ambazo amekwishazichukua hadi sasa katika uongozi wake, alisema amebana matumizi ya serikali kwa kufuta safari zisizo za lazima nje ya nchi, kutumbua watumishi hewa, kutoa elimu bure, na mwezi ujao ndege mbili mpya zitatua nchini kutoka Canada zinaponunuliwa.
Akizungumzia upanuzi wa barabara ya Airport, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe, Janet, alimtaka Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Edwin Ngonyani, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara hiyo hadi Airport, badala ya kuishia Pasiansi, inajengwa haraka iwezekanavyo.
“Upanuzi wa barabara hii usiishie Pasiansi, uende hadi Airport na iwe ni barabara yenye njia nne ili kusudi watalii wanapofika hapa watambue kuwa wameingia jijini Mwanza,” alisema na kuongeza kuwa serikali itatoa fedha za upanuzi wa barabara hiyo hadi Airport na kuahidi kutoa kiasi cha fedha kitakachohitajika ukamilishaji ujenzi wake.
Aidha, alikerwa na ukusanyaji duni wa mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vitega uchumi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka viongozi wote wa chama kuhakikisha kuwa wanakusanya mapato halali yanayolingana na vitega uchumi walivyo navyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ngonyani aliwashukuru wakazi wa Mwanza kwa kazi kubwa waliyofanya ya kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais wa Tanzania.