SIKU moja baada ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kutangaza kuiva kwa Mpango wa Serikali wa kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonya juu ya kuwepo kwa matapeli katika mpango huo.
Amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kujiepusha na matapeli wanaopita katika maeneo yao na kuwataka wachange fedha za kuanzisha vikundi ili wapewe fedha hizo na serikali.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoani Katavi jana, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kukaa macho na matapeli katika fedha hizo maarufu kama mabilioni ya Rais John Magufuli.
“Serikali bado hatujaanza kusambaza fedha hizo. Jihadharini na hao matapeli na wezi hivyo wakija kwenye maeneo yenu wakamateni. Zoezi hilo likianza mtajulishwa kupitia halmashauri zenu,” aliwasisitiza.
Alitoa onyo hilo siku moja baada ya NEEC kutoa onyo kama hilo juzi kwa kusema kumekuwa na taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa kuna baadhi ya taasisi na watu binafsi wanawadanganya wananchi kuwa fedha hizo zitapitia kwenye taasisi zao na kuwataka kujisajili nao ili waweze kufaidika na fedha hizo, jambo ambalo si la kweli.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa alisema fedha hizo zimelenga kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (Saccos) na vikundi vya kifedha vya kijamii vikiwemo Vicoba kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Mpango huo uliobatizwa jina la Fedha za Mfuko wa Mzunguko, unalenga kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.
“Watu na taasisi hizo zinazowadanganya wananchi zimekuwa zikiwatoza viwango mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai ni ada ya usajili ili vikundi hivyo vya wananchi viweze kusajiliwa na kutambuliwa kuweza kufaidika na mamilioni hayo kwa kila kijiji,” alisema Issa.
Kwa wakati tofauti Serikali ya Awamu ya Tano imesisitiza kuwa itakuwa macho ili kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa na kuwafikia walengwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu jana alikagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Kavuu linalojengwa na Kampuni ya Nandra Engineering & Construction Ltd ya Morogoro na kumtaka mkandarasi kulikamilisha haraka. Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa meta 85.34 wenye thamani ya Sh bilioni 2.7 unagharimiwa na serikali kwa asilimia 100.