Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Aug 10, 2016

Majaliwa acharuka

Soko la Mwanjelwa mjini Mbeya.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya kuwepo kwa ubadhirifu katika ujenzi wa Soko la Mwanjelwa.

“Inasikitisha ujenzi wa soko hili kuingia ubabaishaji. Ujenzi wa soko ungegharimu shilingi bilioni 16 ila sasa watendaji wamefanya mambo ya hovyo na kufikia shilingi bilioni 26, hatuwezi kuwavumilia lazima hatua zichukuliwe kwa wote watakaobainika katika ubadhirifu huu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Pia amempa siku tatu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kufanya uchunguzi na kubaini nani aliyetafuna Sh milioni 489 zilizotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya uendelezaji wa soko hilo, ambazo hazijulikani zilipo. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika soko la Mwanjelwa na kubaini ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa soko hilo.
Waziri Mkuu alisema baada ya CAG kumaliza kufanya ukaguzi, atatoa taarifa na mtu yeyote atakayetajwa katika ripoti hiyo kuwa amehusika na ubadhirifu huo, atawajibika hata kama yuko nje ya Jiji la Mbeya.
Alisema kitendo cha kuongeza gharama za ujenzi wa soko hilo kutokana na kuchelewa kwa ujenzi wake, kinaisababishia halmashauri ya jiji kulipa Sh milioni 200 kila mwezi kwa ajili ya marejesho, hivyo aliagiza aliyesababisha gharama hizo asakwe na achukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa Mbeya, Amos Makalla kuhakikisha mtu aliyepangishwa katika kibanda cha kukusanyia uchafu sokoni hapo, anaondolewa haraka na kurudishiwa fedha zake ili kibanda hicho kitumike kama ilivyokusudiwa.
Pia alimuagiza mkuu huyo wa mkoa, kufanya ukaguzi katika vyumba vya maduka sokoni hapo na ifikapo Jumatatu kama mtu hajaweka mali, anyang’anywe na kupangishwa kwa mtu mwingine mwenye kuhitaji.
Alisema hayo baada ya baadhi ya wafanyabiashara, kulalamika kuwa kuna watu wamechukua vyumba vingi vya maduka kwa ajili ya kuvipangisha kwa wafanyabiashara kwa gharama kubwa, tofauti na inayotozwa na halmashauri, hivyo kunyima nafasi kwa walengwa kunufaika na soko hilo.
Mmoja wa wajasiriamali sokoni hapo, Mohammed Said alisema watu wameshika vyumba na kuviuza kwa Sh milioni 20 hadi 40 kulingana na eneo kilipo chumba, jambo linalosababisha baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kupata nafasi katika soko hilo.
Awali, mkuu wa mkoa alisema soko hilo, linakabiliwa na matatizo mbalimbali, kwani hata waathirika waliokuwa wanafanya biashara kabla ya soko kuungua moto mwaka 2006, hawakupewa kipaumbele wakati wa upangishaji wa vyumba vya maduka.
Kuhusu suala la kukosekana kwa wateja, Makalla aliwataka wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyokuwa rasmi kuhamia sokoni mara moja.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP