Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani) amewaagiza wakuu wa wilaya na maofisa elimu nchini, wafanye ukaguzi katika shule ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.
Katika hatua nyingine, serikali imesema itawavua madaraka wakuu wa shule ambao hawataki kubadilika na kuwatimua walimu wote wanaotumia dawa za kulevya ikiwemo bangi, wasio na sifa ya kufundisha na wenye vyeti bandia kwani wamekuwa chanzo cha kudorora kwa ufaulu katika shule kongwe nchini.

Aidha, imeanza kutoa Sh bilioni 21 kila mwezi kama ruzuku ya uendeshaji shule za msingi na sekondari na posho ya madaraka kwa ajili ya wakuu wa shule na walimu wakuu.
Kuhusu kufanyika kwa ukaguzi katika shule ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa Elimu Bure, Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Kila mwezi serikali inapeleka shule zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharimia elimu bure na sasa tumeanza kuona udanganyifu katika sekta ya elimu kwa kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nendeni mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi. “Mkiona takwimu ziwachanganya ni lazima mtoke maofisini na kwenda katika shule zilizo kwenye mpango wa elimu bure mkafanye uhakiki wa idadi ya wanafunzi,” alionya.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema maamuzi yanayotolewa kwenye vikao vya madiwani, lazima yawe na tija na aliitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kuboresha shughuli za maendeleo badala ya kujilipa posho.
“Lazima mjipange vizuri na kupunguza changamoto zinazoikabili wilaya yenu. Malipo yote ni lazima yawe yale yaliyoainishwa katika waraka na si vinginevyo. Mtu wa Ilala unadai nauli ya Sh 200,000, hivi unakuwa unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” Waziri Mkuu alihoji na kushangazwa.
Alisema ni lazima halmashauri zote nchini, zizingatie Sheria za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watendaji wake wajiulize kama mambo wanayoyafanya yana tija na wanawatendea haki watu wanaowatumikia.
Alisema Serikali inataka kuwa na watumishi wanaotambua nafasi zao na watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu pamoja na uwajibikaji mkubwa hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na yenye matokeo chanya.
“Kuna watu wanaona ukuu wa idara ndiyo kila kitu, hata yule anayekimbiza mafaili hathaminiwi, hili si jambo jema, ninyi wote ni kitu kimoja, ni watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja amthamini mwenzake,” alisema na kuongeza; “Mkurugenzi yeyote asikubali kuwa na wakuu wa idara wasiokuwa na ushirikiano na watumishi wengine kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji ndani ya eneo lake.”
Wakuu wa shule kuvuliwa madaraka
Katika hatua nyingine, serikali imesema itawavua madaraka wakuu wa shule ambao hawataki kubadilika na kuwatimua walimu wote wanaotumia dawa za kulevya ikiwemo bangi, wasio na sifa ya kufundisha na wenye vyeti bandia kwani wamekuwa chanzo cha kudorora kwa ufaulu katika shule kongwe nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha kujadili hali ya taaluma katika shule kongwe za sekondari za serikali.
Simbachawene alisema katika matokeo ya mitihani inaonesha taaluma katika shule kongwe inaendelea kushuka kwa baadhi ya shule hizo kuwa za mwisho katika mtihani wa Kidato cha Sita.
Alisema mwaka 2014 shule za sekondari Tambaza na Iyunga zilikuwa za mwisho katika mitihani ya Kidato cha Sita, mwaka 2015 shule ya sekondari Kwiro ilishika nafasi ya mwisho na mwaka 2016 shule ya sekondari Azania imekuwa ya mwisho.
Alisema pia wizara imebaini kuwepo kwa usimamizi dhaifu katika ngazi ya shule na kata, walimu hawasimamii kikamilifu katika utendaji kazi. Pia kutozifanyia kazi taarifa za ukaguzi na maandalizi duni ya walimu kabla ya kufundisha.
“Walimu vijana wamekuwa wakijihusisha na madawa ya kulevya sasa najiandaa kuwatimua walimu wote ambao hawana sifa.” Alisema Tamisemi, itawalinda wakuu wa shule ambao watawataja kwa majina walimu ambao hawastahili kuwa kwenye utumishi.
“Pia wakuu wa shule wazembe ambao hawako tayari kubadilika watavuliwa madaraka sambamba na walimu wanaotumia dawa za kulevya ikiwemo bangi na wasio na sifa ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakichangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika shule kongwe nchini,” alisema.
“Matumizi ya ‘smart phone’ ambazo dunia nzima inakuwa kwenye kiganja, wanafunzi wanamiliki simu hizo, akitaka Whatsapp, akitaka kuingia kwenye intaneti anaona kila kitu kinachotokea, akitaka picha za ngono anaona, akitaka kujua Hollywood kinatokea nini anaona lakini hapo hujazungumzia I miss you, I love you. Msichana akitumiwa meseji hizo kwa siku mara tano hafikirii tena shule,” alisema.
Aliwataka wakuu wa shule, kufanya msako ili kubaini wanafunzi wanaomiliki simu hizo, kwani kwenye shule binafsi wamekuwa wakali sana na kwamba kuna haja ya kutafakari na kuangalia pande zote zenye matatizo. Alisema kumekuwa na tatizo la kutowachukulia hatua walimu wasiowajibika.
“Mwalimu mtoro wa siku 400 au 1,000 badala ya siku tano za kisheria, huu ni uzembe mkubwa wa kiongozi kwa miaka mingi sasa mashauri yanayofikishwa TSD/TSC ni za utoro lakini si za kutofundisha,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Bernard Makali alisema katika matokeo ya Kidato cha Sita miaka mitatu mfululizo, shule 10 za mwisho ni shule kongwe.
Ruzuku, posho juu
Serikali pia imeanza kutoa Sh bilioni 21 kila mwezi, kama ruzuku ya uendeshaji shule za msingi na sekondari na posho ya madaraka kwa ajili ya wakuu wa shule na walimu wakuu.
Waziri akizungumzia hatua hiyo jana, alisema awali serikali ilikuwa ikitoa ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari kiasi cha Sh bilioni 18.77 kwa kila mwezi na sasa inatoa Sh bilioni 21 kwa mwezi kwa kujumuisha posho za wakuu wa shule na walimu wakuu.
“Sasa serikali inatoa Sh bilioni 21 kwa mwezi ikiwa ni ruzuku za uendeshaji wa shule za msingi na sekondari na kwa ajili ya posho za walimu,” alisema.
Alisema kuanzia mwezi huu, wakuu wa shule wataanza kupokea Sh 250,000 kila mwezi ikiwa ni posho za madaraka kwa walimu wakuu wa shule za msingi watapokea Sh 200,000 kila mwezi. Simbachawene alisema fedha hizo zimeshatoka na zimeshafika ili kuwafanya walimu wafanye vizuri.
“Tumenunua pikipiki zaidi ya 1,000 kwa waratibu wa elimu wa kata na mpango huo unaendelea ili kila mratibu awe na usafiri,” alisema na kuongeza kuwa serikali inafanya hivyo ili wananchi waone nguvu kubwa inayowekeza katika sekta ya elimu.
Imeandikwa na Oscar Mbuza, Dar na Sifa Lubasi, Dodoma