Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbarouk
MBUNGE wa Jimbo la Tanga kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mussa Mbarouk amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tanga kujibu shitaka la kutoa maneno ya uchochezi.
Mbunge huyo alifikishwa mahakamani hapo saa 8.30 alasiri jana akiambatana na jopo la mawakili wake wakiongozwa na Warehema Kibaha.

Mbele ya Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Hilda Lyatuu Wakili wa Serikali, Saraji Iboru alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 13, mwaka huu.
Iboru alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo la kutoa maneno ya uchochezi wakati akiwa katika mtaa wa Madina jijini Tanga majira ya saa 10 jioni alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Wakili Siraji akiwa na mwanasheria mwenzake wa Serikali, Shose Naiman aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa katika mkutano huo, Mbunge huyo alisema Mapango ya Amboni yanatumika kwenda kuwaua vijana.
Mshitakiwa huyo alikana shitaka hilo na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi leo ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka na mshitakiwa kukamilisha taratibu za kupata watu watakaokidhi masharti ya dhamana ambayo yamewekwa na mahakama.
Hata hivyo, Mbunge Mbarouk pamoja na mambo mengine leo atatakiwa kuripoti mahakamani hapo akiwa ameambatana na watu wawili ambao ni watumishi wa serikali ambao ndio watakuwa na sifa ya kumdhamini katika shitaka hilo.